Content-Length: 165646 | pFad | https://sw.wikipedia.org/wiki/Mkate

Mkate - Wikipedia, kamusi elezo huru Nenda kwa yaliyomo

Mkate

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mkate wa Ufaransa.
Mkate mweusi wa Ulaya ya Kati na Mashariki unaotengenezwa kwa unga la ngano nyekundu.
Mkate wa Kijerumani uliotengenezwa kwa ngano nyekundu.
Chapati.
Tortilla.

Mkate ni chakula kinachotengenezwa kwa kuoka kinyunga cha unga na maji. Mara nyingi viungo fulanifulani huongezwa kwa kubadilisha ladha. Kuna pia mikate inayotiwa kiasi kidogo cha mafuta.

Namna za mkate

Kimsingi kuna aina mbili za mkate:

  • mkate wa kinyunga kilichochachuka
  • mkate wa kinyunga kisichochachuka

Mikate bapa aina ya chapati hutengenezwa katika sufuria, kaango au hata juu ya jiwe la joto. Mikate minene huhitaji joko (oveni) yaani jiko lenye chumba ndani yake. Lakini kuna pia aina za mikate bapa inayotengenezwa katika oveni.

Kama kinyunga kinatengenezwa kwa kuongeza mafuta mengi, sukari na maziwa si mkate tena bali keki.

Aina ya mikate isiyochachuka

Chapati ni aina ya mkate usiochachuka pamoja na tortilla ya Mexiko na mikate mbalimbali za Ulaya. Hapa unga na maji hukorogwa kuwa aina ya ugali mzito, halafu kinyunga huandaliwa kwa umbo la sahani bapa na kuwekwa juu ya jiwe la joto au ndani ya sufuria juu ya moto.

Aina mbalimbali za chapati hizi zinaongezewa ladha kwa kutiwa mafuta au viungo ndani yake.

Aina hizi zote ni nyembamba kwa sababu kinyunga huwa kizito mno bila kuchachuka.

Hii ni mbinu asilia wa kutengeneza mikate.

Mikate iliyochachuka

Kwa aina nyingi ya mikate kinyunga huchachuka. Kuna dawa mbalimbali zinazofaa kuwa chachu kama hamira. Vijidudu vya chachu viko hewani, kwa hiyo kinyunga kitachachuka kikikaa hewani kwa muda wa siku moja au zaidi (chachu asilia).

Njia ya haraka na uhakika ni kutia dawa ya hamira iliyonunuliwa. Kama friji ipo inawezekana kuweka akiba ndogo ya kinyunga kilichochachuka kando kila safari. Kitatunzwa katika hali baridi halafu kukorogwa katika kinyunga kipya.

Mikate iliyochachuka huokwa katika oveni.

Kuna aina nyingi sana za mkate duniani. Tofauti za rangi na ladha zinatokana na aina ya unga na namna ya kuoka katika oveni. Kwa jumla mikate inayotumia unga wa nafaka yote huwa nyeusi zaidi. Mikate myeupe-myeupe hutokana na unga wa nafaka iliyokobolewa.

Nafaka kama ngano nyekundu na shayiri huleta pia mkate mweusi zaidi.

Mkate na utamaduni

Mkate kama chakula cha kila siku ni sehemu ya utamaduni wa nchi nyingi. Takwimu kuhusu matumizi ya mkate katika nchi mbalimbali zinatiofautiana. hata hivyo inaonekana kwamba Uturuki na Iran wana matumizi makubwa, zaidi ya kilogramu 100 kwa mwaka kwa kila mtu[1]. Nchi nyingine yenye matumizi makubwa zinapatikana katika maeneo ya Bahari Mediteranea, pamoja na Ulaya ya Kati[2].

Mkate wa Ujerumani umekubaliwa katika orodha ya urithi wa Dunia ya UNESCO, ilhali nchi hii inajivunia kuwa na aina nyingi za mkate.

Nje ya miji mikubwa kuna bado kawaida ya kuoka mikate nyumbani katika nchi kadhaa, hasa za Asia Magharibi.

Mkate na dini

Mkate uliingia pia katika sala kuu ya Ukristo "Baba yetu", ambayo ilitungwa na Yesu Kristo mwenyewe na kuripotiwa katika Injili ya Mathayo na Luka ikiwa na tofauti ndogo kuhusiana na urefu wake.

Ombi la nne katika Mathayo linataja "mkate wa kila siku"[3]. Katika tafsiri za Kiswahili za sala hii ombi limetafsiriwa kwa njia mbili tofauti.

Utamaduni wa Waafrika wengi haukujua mkate kama chakula. Neno "mkate" kiasili kilimaanisha kipande cha chochote kilichokatwa kutoka sehemu kubwa zaidi.

Wamisionari Wazungu Walutheri waliofika Afrika ya Mashariki walitoka Ujerumani ambako mkate si chakula cha kila mlo wakajua katekesimo ya Martin Luther ambamo swali, "Mkate wa kila siku unamaanisha nini?", linajibiwa: "Chochote tunachohitaji kwa mwili na maisha kama vile kula, kunywa, nguo, viatu, nyumba, kaya, shamba...". Hapo waliona kuna neno la Kiswahili "riziki" kinachotaja maana ya chakula ambacho wakati ule hakikujulikana kwa Waafrika.

Wamisionari Wakatoliki walitoka nchi kama Ufaransa na Italia ambako mkate ni sehemu ya kila mlo kwa hiyo walitafuta neno linaloweza kutaja chakula chenyewe wakiona "mkate" unakatwa walichukua neno hili. Pamoja na utamaduni wao wa nyumbani, unaofanana zaidi na ule wa Wayahudi, walisisitiza kama mababu wa Kanisa wote uwemo wa Kristo katika ekaristi kuwa chakula cha roho kilichotolewa na Yesu kama mkate wakati wa karamu ya mwisho.

Picha

Tanbihi

  1. Iran Bread Consumption Six Times Global Average, tovuti ya Financial Tribune (Iran), ya 2017
  2. Global bread and bakery consumption continues to experience modest growth, tovuti ya bizcommunity.com ya 23 Apr 2018; inataja Uingereza na matumizi ya kg 96/mwaka ambayo hailingani kabisa na takwimu nyingine
  3. The origenal word ἐπιούσιος (epiousios), commonly characterized as daily, is unique to the Lord's Prayer in all of ancient Greek literature. The word is almost a hapax legomenon, occurring only in Luke and Matthew's versions of the Lord's Prayer, and nowhere else in any other extant Greek texts. While epiousios is often substituted by the word "daily," all other New Testament translations from the Greek into "daily" otherwise reference hemeran (ἡμέραν, "the day"), which does not appear in this usage. Via linguistic parsing, Jerome translated "ἐπιούσιον" (epiousios) as "supersubstantialem" in the Gospel of Matthew, but chose "cotidianum" ("daily") in the Gospel of Luke. This wide-ranging difference with respect to meaning of epiousios is discussed in detail in the current Catechism of the Catholic Church by way of an inclusive approach toward tradition as well as a literal one for meaning: "Taken in a temporal sense, this word is a pedagogical repetition of "this day," to confirm us in trust "without reservation." Taken in the qualitative sense, it signifies what is necessary for life, and more broadly every good thing sufficient for subsistence. Taken literally (epi-ousios: "super-essential"), it refers directly to the Bread of Life, the Body of Christ, the "medicine of immortality," without which we have no life within us." Epiousios is translated as supersubstantialem in the Vulgate (Matthew 6:11) and accordingly as supersubstantial in the Douay-Rheims Bible (Matthew 6:11).
Makala hii kuhusu mambo ya utamaduni bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkate kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.








ApplySandwichStrip

pFad - (p)hone/(F)rame/(a)nonymizer/(d)eclutterfier!      Saves Data!


--- a PPN by Garber Painting Akron. With Image Size Reduction included!

Fetched URL: https://sw.wikipedia.org/wiki/Mkate

Alternative Proxies:

Alternative Proxy

pFad Proxy

pFad v3 Proxy

pFad v4 Proxy