Content-Length: 93243 | pFad | https://sw.wikipedia.org/wiki/Sokotra

Sokotra - Wikipedia, kamusi elezo huru Nenda kwa yaliyomo

Sokotra

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Ramani ya kisiwa cha Sokotra
Mahali pa Sokotra kati ya Afrika na Bara Arabu

Sokotra (Kar: سقطرى suquṭra) (iliyojulikana zamani kama Mahara) ni funguvisiwa ndogo ya Yemen katika Bahari Hindi kati ya Somalia na Bara Arabu. Sokotra ni hasa jina la kisiwa kikubwa cha funguvisiwa hii.

Jiografia

[hariri | hariri chanzo]

Kijiolojia funguvisiwa ni sehemu ya Afrika lakini kiutamaduni na kihistoria ni sehemu ya kusini ya Bara Arabu. Kiutawala ni sehemu ya wilaya ya 'Adan ya jamhuri ya Yemeni.

  • Kisiwa kikuu cha Sokotra kina eneo la 3,579 km² na wakazi 80,000.
  • Visiwa vitatu vya Abd al-Kuri (162 km² na wakazi 300), Samha (45 km² na wakazi 100) na Darsa (10 km², haina wakazi)

Umbali kati ya Adb al-Kuri hadi Somalia ni takriban 100 km.

Hali ya hewa ni kama jangwa.

Karibu miji na vijiji vyote viko kwenye pwani la kaskazini. Katikati kuna milima makavu inayofikia kimo cha 1,500 m juu ya UB. Makao makuu ni mji wa Al Hadibu (au: Tamrida) wanapokaa zaidi ya nusu ya wakazi ya kisiwa chote (takriban watu 45,000 - 50,000). Uwanja wa ndege mpya umejengwa karibu na Qadub.

Mabonde ya pwani yana nafasi ya mimea inayowezesha ufugaji wa ng'ombe na mbuzi. Kuna pia maeneo madogo kwa mashamba. Menginevyo wenyeji tangu zamani huvuna uvumba kutoka miti ya kieneyeji na kuuuza nje. Wengi hupata maisha kama wavuvi.

Historia

[hariri | hariri chanzo]

Sokotra imejulikana tangu zamani za Wagiriki wa Kale kama kituo cha biashara kati ya nchi za Bahari ya Shamu na Uhindi. Katika Periplus ya Bahari ya Eritrea inaitwa "Dioskouridou". Mtaalamu G.W.B. Huntingford amedai ya kwamba asili ya jina ni lugha ya Kihindi Sanskrit "dvipa sukhadhara" (kisiwa cha heri).

Sokotra ilijulikana kwa karne nyingi kama kisiwa cha Wakristo wa dhehebu la Kisiryan cha Mashariki (Kinestorio). Msafiri Mwarabu Abu Mohammed Al-Hassan Al-Hamdani aliandika wakati wa karne ya kumi BK ya kwamba idadi kubwa bado walikuwa Wakristo. Mnamo 1507 Wareno walitwaa mji mkuu wa Suk ikaonekana Wakristo kahdaa bado walikuwepo. Taarifa za karne ya 19 zaonyesha ya kwamba wakazi wote walikuwa Waislamu.

Baada ya kuondoka kwa Wareno funguvisiwa ikatawaliwa na masultani wa Mahra katika kusini ya Bara Arabu tangu 1511. Pamoja na usultani huu kisiwa kilifika chini ya utawala wa Kiingereza baada ya 1866. Wakati wa uhuru wa Yemen ya Kusini mwaka 1966 usultani ulifutwa ukawa sehemu ya Yemen Kusini pamoja na Sokotra. Leo hii imekuwa sehemu ya Yemen iliyounganishwa.

Hadi leo wenyeji wanatumia luha ya pekee ya Kisokotra ambayo ni lugha ya Kisemiti inayofanana na lugha nyingine za Bara Arabu Kusini katika Yemen na Dhofar.









ApplySandwichStrip

pFad - (p)hone/(F)rame/(a)nonymizer/(d)eclutterfier!      Saves Data!


--- a PPN by Garber Painting Akron. With Image Size Reduction included!

Fetched URL: https://sw.wikipedia.org/wiki/Sokotra

Alternative Proxies:

Alternative Proxy

pFad Proxy

pFad v3 Proxy

pFad v4 Proxy