Waklara
Waklara ni jina linalojumlisha wanawake wote waliomfuata utawani Fransisko wa Asizi (1182-1226) nyuma ya Klara wa Asizi (1193-1253).
Mche mdogo ulivyostawi (1212-1517)
[hariri | hariri chanzo]Mwanzo na uenezi (1212-1300)
[hariri | hariri chanzo]Klara, aliyejiita “mche mdogo wa Mt. Fransisko”, ndiye jiwe la msingi la Utawa II wa Wafransisko ulioleta karama ileile ya Ndugu Wadogo kwa wanawake na kwa kujifungia faraghani. Ndizo nguzo mbili za utawa huo.
Binti huyo wa ukoo bora alizaliwa Asizi (Italia) mwaka 1193. Kisha kuvutiwa na mifano ya Fransisko, na kusikiliza mahubiri na mashauri yake, akaamua kujiweka wakfu kwa Yesu Kristo katika ufukara mkuu. Basi, akatoroka nyumbani usiku (1212) akamuendea Fransisko huko Porsyunkula ambapo alinyolewa naye na kuvikwa kanzu, kamba na shela nyeusi. Kesho yake asubuhi akapelekwa kwa masista Wabenedikto, na baada ya wiki mbili kwenye monasteri yao nyingine, alipofikiwa na mdogo wake (Anyesi wa Asizi) ambaye pia alipaswa kukabili upinzani mkali wa ukoo wao.
Fransisko alipomaliza kuandaa jengo la Mt. Damiano, akina dada hao wakahamia huko kushika maisha ya ndani, wakaongezeka haraka. Miaka 40 baadaye Klara akaja kuandika kwamba mwanzo ulikuwa mgumu na walidharauliwa sana. Mwaka huohuo (au ule uliofuata) mwanzilishi, alipoona walivyovumilia yote, aliwaandikia kwa ufupi “mtindo wa maisha”. Wakati huo aliwaomba wamsaidie kutambua kama Mungu anataka yeye na Ndugu Wadogo waishi upwekeni tu au wafanye utume pia. Jibu likawa kwamba wakahubiri; lakini Klara na wenzake watawafuata kiroho tu kwa sala na sadaka, wakichangia urekebisho wa Kanisa bila ya kutoka nje ya kiota chao.
Baada ya Mtaguso IV wa Laterano (1215) kukataza kanuni mpya iliwabidi wapokee mojawapo ya zamani ili wakubaliwe na Kanisa Katoliki kama watawa. Basi wakaichagua ile ya Benedikto wa Nursia, wakiifuata katika mambo kadhaa kadiri yalivyopatana na mtindo wao mpya, bila ya nia ya kuwa Wabenedikto. Hapo ilimpasa Klara kuitwa abesi, jina alilolikubali tu kwa kumtii mwanzilishi, ingawa akaendelea kujiita “mtumishi wa Kristo na wa akina dada fukara”. Hasa Klara hakutosheka na uhalali wa monasteri yake mbele ya Kanisa, bali kwa njia ya Fransisko aliomba akapewa na Papa Inosenti III “fadhili ya ufukara” (1216), yaani ruhusa ya kuishi bila ya mali hata kijumuia, kama jambo la msingi katika wito wake wa “kuishi kadiri ya ukamilifu wa Injili takatifu”, kwa kuungana na Yesu fukara kama bibiarusi fukara.
Kardinali Ugolino, akiona monasteri za namna hiyo zinavyoongezeka huko na huko, alizitungia katiba (1219) iliyopitishwa na Papa Honori III (1216-1227) ambayo ikawa msingi wa kanuni zote zilizoandikwa baadaye kwa Utawa II. Lengo lake lilikuwa kukinga monasteri hizo dhidi ya upinzani na kuzipa mtindo wa kimonaki zaidi bila ya kuondoa usahili wake maalumu, ziwe muundo mpya wa aina moja chini ya Kanisa la Roma moja kwa moja. Katika juhudi zake za kurekebisha umonaki alielekeza hata monasteri kadhaa za zamani zifuate mtindo wa Mt. Damiano. Desturi kali alizoziagiza humo hazikumtisha Klara, ambaye alijishinda tayari na kujitesa kwa ushujaa mkubwa (katika kula, kuvaa, kulala n.k.) mpaka akakatazwa asizidishe. Wala hakuogopa ukali wa ugo ulioagiwa na katiba hiyo, ili kutunza mazingira ya sala. Wasiwasi wake ulihusu ufukara mkuu akiona hautajwi na katiba hiyo. Mwanzoni Ugolino alitaka msimamo huo udumu katika monasteri kadhaa, ila alipochaguliwa kuwa Papa akaanza kuzipatia mali nyinginyingi, labda kisha kung’amua matatizo yaliyojitokeza. Lakini Klara hakukubali kabisa akamuomba amtibitishie “fadhili ya ufukara” akakubaliwa (1228), lakini si kwa monasteri zote.
Suala lingine lililojitokeza mapema, halafu likaendelea kusababisha migogoro, ni nani awajibike kuwasaidia Waklara upande wa roho na upande wa riziki. Fransisko alipokuwa Mashariki, Filipo Longo aliteuliwa msimamizi wao, lakini mwanzilishi aliporudi uteuzi huo ukafutwa, masista wakasimamiwa tena na wasio Wafransisko, mpaka Ugolino, kisha kuchaguliwa awe Papa Gregori IX (1227-1241) alipowalazimisha Ndugu Wadogo kuwajibika (1221).
Klara alipoona wito wake wa Kiinjili upo hatarini upande wa sheria, kwa kuwa kanuni na katiba hazikuwa za Kifransisko, akaanza kuomba aweze kuahidi kushika kanuni ya Ndugu Wadogo badala ya ile ya Benedikto. Mwaka 1234 akaja kumuunga mkono Anyesi wa Praha, binti mfalme ambaye alikataa kuolewa na mfalme mkuu Federiko II wa Ujerumani akaanzisha monasteri yake iliyokubaliwa “fadhili ya ufukara”. Alitunga kanuni mpya kwa kuchanganya “mtindo wa maisha” alioandika Fransisko na katiba ya Ugolino, akamuomba Gregori IX, halafu Papa Inosenti IV (1243-1254) waithibitishe, lakini akakataliwa. Kumbe Inosenti IV akathibitisha katiba ya Ugolino (1245) na kusisitiza ifuatwe kanuni ya Benedikto kwa sababu ina sifa nyingi. Wakati huohuo alijaribu kusuluhisha mgogoro wa uhusiano kati ya Ndugu Wadogo na Waklara. Klara alikuwa akiendelea kudai kwa nguvu msaada wa kiroho wa ndugu hao kulingana na ahadi ya mwanzilishi. Kumbe Mtumishi mkuu Kreshensi wa Iesi (1244-1247) aliomba shirika liondolewe mzigo liliobebeshwa na Gregori IX, yaani himizo la kuanzisha konventi ndogo karibu na kila monasteri ya Waklara. Basi, Inosenti IV aliamua Waklara wawe chini ya uongozi na mamlaka ya Ndugu Wadogo, akapendekeza masista waunganishwe na Utawa I. Lakini shirika likazidi kuona litalemewa na wingi wa monasteri.
Mwaka 1247 Inosenti IV akatunga katiba mpya badala ya ile ya Ugolino iliyokwishaenea katika monasteri zote za Kifransisko, ikitumika pengine pamoja na desturi maalumu za mahali. Katiba hiyo ilifanya kanuni ya Ndugu Wadogo kuwa msingi wa sheria za Waklara bila ya kuwadai waishike katika yote, ila katika utiifu, utovu wa mali na useja mtakatifu. Katiba hiyo ilimuondolea Kardinali mlinzi mamlaka juu ya Waklara, ambao wakawekwa moja kwa moja chini ya viongozi wa Utawa I. Kwa katiba hiyo Waklara wakaja kutambulikana Wafransisko kisheria, lakini ndani mlikuwa na pigo kubwa kwa Klara, yaani iliandikwa wazi kuwa monasteri zao zinaruhusiwa kuwa na mali za kujitegemea. Ndiyo sababu monasteri chache tu zikaipokea katiba hiyo. Vilevile Ndugu Wadogo wakazidi kulalamika hadi Kardinali mlinzi akajitwalia polepole mamlaka yao na hatimaye (1250) aliwaandikia wasithubutu kujiingiza katika uongozi wa Waklara. Hivyo kwa muda mfupi katiba hiyo ikashindikana pande zote.
Klara, mgonjwa toka siku nyingi, alipoona kifo kinamkaribia, aliandika wasia wake ambamo alimuiga Fransisko katika kukumbusha asili ya wito wake na wa jamaa yake, na kutamka kwa msisitizo mkubwa nia imara ya kufuata ufukara mkuu “aliouahidi kwa Mungu na kwa Mt. Fransisko” pamoja na kuhimiza sana umoja wa dada zake. Lakini pia, upande wa sheria, aliona haja ya kutunga upya “mtindo wa maisha” kwa kulinganisha kanuni ya Ndugu Wadogo na masharti ya maisha ya ndani tu. Humo aliingiza pia maandishi mawili mafupi ya Fransisko kwao, kuhusu ufukara mkuu na kuhusu ahadi ya kwamba yeye na Ndugu Wadogo watawahudumia Waklara sawa na wenzao wa kiume. Upande wake Klara aliahidi kuwatii waandamizi wa mwanzilishi. Kiini cha huo “mtindo wa maisha” kinasisitiza kwa nguvu nia ya kuishi bila ya mali yoyote, isipokuwa monasteri na bustani. Jambo lingine linalokazwa ni udugu: humo neno “dada” linapatikana mara 66! Udugu huo unatimizwa siku kwa siku chini ya “abesi na mama” kwa umoja wa mioyo pasipo ubaguzi wowote (tofauti pekee ni kati ya wanaojua na wasiojua kusoma kuhusu Sala ya Kanisa). Hata dada “wa nje” (yaani “wanaohudumia nje ya monasteri” bila ya kubanwa na ugo) washiriki maisha ya jumuia sawa na wenzao. Hao ni kundi maalumu la mtindo wa Kiklara, linalohitajika kadiri wenzao wanavyojifungia ndani: ni “akina Marta” kwa “akina Maria” kadiri Fransisko alivyowapangia Ndugu Wadogo wanaoishi upwekeni. Udugu huo unajitokeza hata katika mikutano, ambayo inatakiwa kufanyika kila wiki kwa mchango wa wote, kupanga shughuli za maana na kuteua watakaoshika nyadhifa mbalimbali. Abesi mwenyewe, ingawa anachaguliwa kwa maisha yake yote, kadiri ya mapokeo ya kimonaki, anaweza kubadilishwa na dada zake wakiona hawezi kutimiza vizuri kazi zake. Uhusiano na Utawa I unasisitizwa tena kwa kudai msimamizi wa monasteri awe daima Ndugu Mdogo, pamoja na kuomba Utawa huo uipatie monasteri mapadri 2 na mabradha 2 kwa huduma za kiroho na za kimwili.
Huo “mtindo wa maisha” ukakubaliwa na Kardinali mlinzi (1252) halafu na Inosenti IV (1253). Klara akapewa hati yake kitandani akaibusu; siku mbili baadaye akafa akiishika mikononi, wakihudhuria Leo, Angelo na Ginepro, “wenzi watatu” wa Fransisko; pia alijaliwa faraja za [[Bikira Maria na wanawake watakatifu kadhaa. Mazishi yalihudhuriwa na Papa, Makardinali, Maaskofu na wengineo. Inosenti IV alitaka ziimbwe sala za watakatifu mabikira badala ya zile za wafu, ila akakubali shauri la Kardinali mlinzi la kufuata taratibu zilizopangwa kabla mtu hajatangazwa mtakatifu.
Miaka miwili baadaye, Kardinali huyo akiwa amechaguliwa kuwa Papa Aleksanda IV (1245-1261), akamtangaza rasmi kuwa mtakatifu (1255). Mwaka 1260 masalia yake yakahamishiwa mjini Asizi katika kanisa lililojengwa kwa heshima yake.
Pamoja na kanuni na wasia, Klara ametuachia walau barua nne (kwa Agnes wa Praha). Maandishi hayo ndiyo chemchemi ya kwanza ambamo tuchote utajiri wa roho yake na wa utu wake. Hasa ya mwisho inatuonyesha alivyogeuka ndani ya Yesu kwa kuzidi kumkazia macho kama kioo chake na kujifunza toka kwake hasa ufukara, unyenyekevu na upendo wa ajabu, vilivyong’aa katika hatua mbalimbali za maisha yake kuanzia Bethlehemu hadi Kalivari. Klara alimfikia Mungu kwa kumfuata Yesu kama bibiarusi mwaminifu katika hatua hizo za maisha yake halisi, kama alivyoelekezwa na Fransisko, kadiri ya karama yake mpya katika kumtazama Yesu na kuelewa Injili.
Katika karne XIII monasteri chache ziliipokea kanuni ya Klara iliyothibitishwa kwa ajili ya nyumba asili tu. Kumbe monasteri kadhaa zikaja kupokea kanuni maalumu ambayo Izabela (+1270), dada wa mfalme Ludoviko IX wa Ufaransa, aliiandika akakubaliwa na Aleksanda IV kwa monasteri yake ya Longchamp (1259). Kanuni hiyo iliweka Waklara chini ya Ndugu Wadogo na kukubali mali na mapato ya mara kwa mara. Mwaka 1263 mkutano mkuu wa Ndugu Wadogo ulizidi kukataa wajibu wa kuwahudumia Waklara.
Akiwa Mtumishi mkuu, Bonaventura wa Bagnoregio (1257-1274) alijaribu kusuluhisha kwa kusema huduma za kiroho kwa dada hao zinatokana na upendo, lakini si wajibu ambao waudai kwa haki; pia zitegemee uamuzi wa Kardinali mlinzi. Kumbe mwaka huohuo Papa Urbani IV (1261-1264) alipitisha kanuni mpya ili kustawisha nidhamu na umoja ikidai monasteri hizo zote ziitwe Utawa wa Mtakatifu Klara (O.S.C.), kama ilivyoelekea kufanyika baada ya kutangazwa mtakatifu. Kanuni mpya ilifuata kidogo ile ya Klara, na zaidi katiba ya Inosenti IV, ikibana sana masista katika vipengele vingi. Zaidi ya hayo ilipanga mali (mashamba na kodi zake) kuwa tegemeo la kawaida la uchumi wa monasteri. Hatimaye iliwaondolea Watumishi wa kiume wajibu wa kuwahudumia Waklara. Kanuni hiyo ikakataliwa na monasteri bora na baadhi ya Ndugu Wadogo. Hivyo ukatokea mgawanyiko unaodumu hadi leo kati ya Waklara wanaofuata kanuni ya Klara (inayoitwa kanuni I) na wale wanaofuata kanuni ya Urbani IV (Waurbani au wa kanuni II), na kufanana na Wakonventuali (ambao pia wamekubali kuwa na mali kishirika). Kanuni nyingine zikaachwa kabla ya karne kwisha. Kwanza ilienezwa sana ile ya Urbani, lakini ile ya mt Klara ikabaki huko na huko ikiendelea kuathiri sana historia yote ya Waklara kwa kukumbusha tunu asili na kuchochea marekebisho mengi kuliko yale ya Ndugu Wadogo, kutokana na urahisi wa kubadili hali ya monasteri moja kuliko ya shirika kubwa iliyotawanyika sehemu mbalimbali.
Tofauti hizo hazikuzuia uenezi wa monasteri usiende kasi ajabu, kulingana na uenezi wa Utawa I Ulaya na hata ng’ambo ya Bahari ya Kati. Kila monasteri ilijitegemea kikamilifu upande wa mamlaka; kilichowaunganisha ni hakika ya kutokana na moto ule uliowashwa na Klara, uhusiano wa kiroho na Ndugu Wadogo na mamlaka ya Kardinali mlinzi. Kwa kawaida monasteri zilikuwa na masista wengi sana. Miito mingi ilitokea kati ya koo maarufu na za kifalme pia, hasa Urbani IV alipodai kila mtakaji alete “mahari” monasterini, sheria ambayo ilienea kote. Karne ya kwanza ilizaa watakatifu 4 (Klara na Anyesi wa Asizi, Anyesi wa Praha na Kinga wa Hungaria) na wenye heri 6 katika nchi mbalimbali, hasa kutoka koo za kifalme. Halikukosekana taji la ushahidi wa imani na wa ubikira (Waklara wote wa Tripoli mwaka 1289, na wote 70 wa Tolemais mwaka 1291).
Takwimu ni kama ifuatavyo: Mwaka 1253: monasteri 111: Italia + visiwa 68, Hispania + Ureno 21, Ufaransa 14, Ujerumani + Ulaya Mashariki 8. Mwaka 1300: Waklara zaidi ya 15,000 katika monasteri 413: Italia + visiwa 196, Hispania + Ureno 57, Ufaransa 68, Ujerumani + Ulaya Mashariki 46, Mashariki + Korasia 23, Uingereza + Irelandi 23.
Ulegevu (1300-1400)
[hariri | hariri chanzo]Karne XIV ilileta ulegevu katika Utawa II, kama tulivyoona kwa ule wa kwanza, hasa kutokana na wingi wa masista na wa mali. Walipokewa kwa urahisi wanawake wasiofaa lakini wenye kuleta mahari kubwa, ambao waliingiza monasterini watumishi wao binafsi, hata kuleta anasa, pengine kwa idhini ya Papa. Uovu ulizidi wakati wa farakano la Magharibi na fujo iliyofuata. Hata hivyo si monasteri zote zilipatwa kwa pamoja, kutokana na kila moja kujitegemea. Hazikukosekana pia juhudi za kurudisha nidhamu zilizofanywa na wasimamizi wa Utawa I – ambao Papa Bonifas VIII (1295-1303) aliurudishia wajibu wa kuwahudumia Waklara (1296) – na Makardinali walinzi na Mapapa wenyewe. Kati yao ni muhimu hasa Papa Benedikto XII (1334-1342), aliyekuwa mmonaki wa Citeaux, ambaye aliwapa Ndugu Wadogo katiba (1336) ambayo sura yake mojawapo inahusu Waklara tu. Katiba yake ilibadili sura ya monasteri. Kwanza ilipanga idadi ya juu ya masista katika kila monasteri; pili ilisisitiza ugo wa Kipapa, taratibu za pamoja kwa wote, usimamizi mzuri wa mali, katazo la pesa za binafsi na la dhuluma dhidi ya monasteri; tatu alilazimisha hata dada waliohudumia nje ya ugo wabaki ndani na hivyo wakaja kuwa tabaka la chini la masista, wakiwatumikia wenzao bila ya kuwa na sauti mikutanoni (ilikuwa hivyo kwa Wabenedikto, lakini ni kinyume cha udugu alioutaka Klara); nne kwa huduma hizo za nje waliruhusiwa wanawake wasekulari wa kufaa; tano vilikatazwa vyumba vya binafsi.
Jambo lingine lililokuja kubadilishwa ni muda wa uongozi wa abesi, kwa kuzingatia kwamba urefu wake unaweza ukafaa wakati wa juhudi, lakini unaweza ukasababisha uharibifu wa kudumu ulegevu ukiingia. Mtindo wa maisha wa Klara hausemi abesi adumu muda gani, ila unafuata kanuni ya Fransisko ukisema asipofaa tena aondolewe, halafu achaguliwe mwingine. Lakini utekelezaji wake haukuwa rahisi. Hivyo Papa Inosenti VII (1404-1406) aliagiza (1405) abesi achaguliwe kila baada ya miaka 10; baadaye muda ukapunguzwa tena hadi miaka 3. Lakini sheria hizo hazikufuatwa popote, hivyo baadhi ya monasteri zikaendelea kumchagua abesi hadi atakapokufa.
Pamoja na juhudi hizo na nyingine za kurekebisha hali, historia ya utawa inaonyesha kwamba nidhamu ya kuzalimishwa inaweza ikasaidia kiasi, lakini haiwezi kuleta hali mpya, kwa kuwa uhai unatoka ndani ya watawa wenyewe kwa kazi ya Roho Mtakatifu. Si suala la miundo, bali la roho. Hata katika ulegevu wa karne XIV mtindo wa maisha wa Klara ulivutia: kwa mfano malkia Sancha wa Napoli (+1345), alipojifanya Mklara hakukubali kuingia monasteri ya fahari ya Mt. Klara mjini, bali alianzisha nyingine ndogo fukara kwa kuita wamonaki toka Asizi na kushika kanuni I. Huko na huko Ufaransa ilitokea vilevile. Katika karne hiyo walipatikana wenye heri 3.
Takwimu ni kama ifuatavyo: Mwaka 1385: Waklara zaidi ya 15,000 katika monasteri 404: Italia + visiwa 245, Hispania + Ureno 51, Ufaransa 39, Ujerumani + Ulaya Mashariki 50, Mashariki + Korasia 11, Uingereza + Irelandi 8.
Marekebisho kuanza (1400-1517)
[hariri | hariri chanzo]Karne XV hadi XVIII ziliona monasteri za Waklara kuhuishwa tena, kufuatana na marekebisho ya Ndugu Wadogo (kama ilivyotokea kwa wanawake wa mashirika mengine), halafu na Mtaguso wa Trento na maagizo ya Mapapa, lakini pia kutokana na karama yenyewe ya Klara iliyojitokeza wazi katika kanuni yake. Toka mwanzo utawa wake haukuwa tu muundo mpya wa kimonaki, bali mfumo mpya wa maisha ya Kiinjili, ambao unadai kufuatwa, la sivyo monasteri hazitatulia, kama vile Ndugu Wadogo.
Mwanzoni mwa karne XV ulitokea urekebisho mkubwa kwa njia ya Koleta Boylet (+1447) wa Corbie (Ufaransa). Baada ya kujifungia ndani amevaa mavazi ya Wafransisko Wasekulari, alitokewa mara kadhaa na Fransisko na kuhimizwa arekebishe utawa wake.
Basi, akatoka (1406) akaenda kwa Papa wa Avinyon (bila ya kutambua kwamba ni wa bandia) akaweka mikononi mwake nadhiri ya kushika mtindo wa maisha wa Klara, akafanywa naye abesi na mrekebishaji wa utawa wote wa Fransisko (I-II-III), kutokana na karama yake wazi ya kurekebisha Kanisa kuanzia monasteri na miundo mingine ya Kifransisko. Kwa neema ya Mungu na kwa msaada wa wakuu wa dunia akaanza kutembelea Ufaransa na Benelux ili kueneza chachu ya Kiinjili, hasa ufukara. Upande wa Waklara alirekebisha au kuanzisha monasteri 22 kufuatana na kanuni I aliyoomba nakala yake halisi kwa monasteri mama ya Asizi. Mwenyewe aliiongezea katiba iliyopitishwa na Mtumishi mkuu (1432) halafu ikathibitishwa na Papa Pius II (1458-1464). Humo alikataza mahari za masista, mali yoyote na mapato ya hakika kwa monasteri, kodi na ghala za kutosha muda mrefu, kila kitu cha thamani au kisicho cha lazima, majengo yasiyo duni. Aliagiza wote wafanye kazi ili kupata riziki, bila ya kuagiza watu wa nje kwa kazi wanazoweza kuzifanya wenyewe. Kwa udogo, alikataza baraka kuu kwa abesi na ibada ya kuweka wakfu mabikira. Hata hivyo alisisitiza usafi na masomo na kupunguza masharti ya ugo. Kwa ajili ya upendo wa kidugu alifuta matabaka, aliagiza vipindi vya burudani (maongezi), alisisitiza mikutano ya kila wiki, alionyesha tena kuwa wadhifa wowote ni utumishi tu. Ingawa alikubali vipengele kadhaa vya kanuni ya Urbani IV vilivyopata kuwa vya kawaida, kwa jumla alirudia vizuri karama ya Klara. Kama yeye alitaka mafungamano imara na Utawa I, monasteri zote zikiwa chini ya Ndugu Wadogo, na wanne kati yao wakiwa tayari kuihudumia kila mojawapo. Kwa sababu hiyo, kama tulivyokwishaona, watawa kadhaa wa kiume waliingia katika juhudi zake za urekebisho (Ndugu Wadogo Wakoleta).
Ndugu Wadogo Waoservanti mwanzoni walikataa kuwahudumia Waklara, lakini polepole wakalazimishwa na Kanisa kwa ombi la monasteri zilizorekebishwa. Hapo urekebisho wa kina ukapamba kwa juhudi za wamonaki bora, kama Katerina wa Bologna (+1463), Antonia wa Firenze (+1472), Eustokia Calafato (+1485) na Batista Varano (+1524) huko Italia, na wengineo Ufaransa na Hispania. Wote walishikilia kanuni I sio tu kwa Waurbani, bali pia kwa monasteri nyingi za Utawa III na hata nyingine zisizokuwa za Kifransisko! Si zote zilikubali kwa ridhaa yao urekebisho. Kumbe Waoservanti walijaribu kuueneza kote, hata kwa mabavu, mpaka walifikia hatua ya kutumia nguvu za kijeshi kupitia serikali! Kati ya wote aliyejitahidi zaidi ni Yohane wa Capestrano, ambaye alitaka pia kuunganisha monasteri zote chini ya Waoservanti, lakini akashindana na msimamo wa Koleta aliyetaka kubaki chini ya Mtumishi mkuu na kudumisha uhusiano na Wakonventuali. Yohane akaandika (1445) ufafanuzi wa kanuni ya Klara akiorodhesha amri mia na zaidi, jambo lililowashangaza sana Waklara, hata mwaka uliofuata ulitolewa ufafanuzi mwingine juu ya maana ya amri hizo, halafu Papa Eugeni IV (1431-1447) akatamka kwamba chache tu zinawabana masista kiasi cha kutenda dhambi wakizivunja (1447). Mwenyewe aliweka chini ya Waoservanti monasteri zote zilizorekebishwa, hata zikifuata kanuni II, akiziacha nyingine chini ya Mtumishi mkuu. Kwa maana sera ya Kanisa haikuwa kulazimisha monasteri kufuata kanuni I, ila kuzirekebisha kwa kufuata sawasawa sheria za kila mojawapo; pengine waliokataa urekebisho iliwabidi wahame. Mwishoni mwa karne XV Waklara wa urekebisho wakawa wengi kuliko wasiorekebishwa. Sehemu nyingine monasteri za hawa wa mwisho zilikuwa na hali mbaya kweli. Hatimaye baadhi ya zile zilizokataa urekebisho zilibadili kanuni na kufuata ile ya Benedikto. Jambo lingine lisilopendeza lilikuwa kuona Waoservanti na Wakonventuali wakishindania monasteri za dada zao.
Kati ya marekebisho hayo, Wakoleta wamedumisha hadi leo umoja fulani kati ya baadhi ya monasteri zao. Vilevile Waklara Pekupeku walioanzishwa na Marina wa Villaseca (Hispania) aliyeruhusiwa (1490) kurekebisha monasteri yake ya Utawa III kwa kufuata kikamilifu kanuni I, na kupokea Waurbani wasirudie unovisi. Makundi mengine yamepoteza umaalumu wao: kwa mfano Dada Fukara Waklareno ambao Papa Sisto IV (1471-1484) aliwaweka (1473) chini ya Mtumishi mkuu kumpitia makamu wake Mklareno.
Papa Inosenti VIII (1484-1492) alimruhusu (1489) Beatriche wa Silva Meneses (+1490) aunde monasteri ya Kibenedikto aina ya Citeaux kwa heshima ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili (Imaculata Concepcion). Baada ya mwanzilishi kufariki, Papa Aleksanda VI (1492-1503) akawaruhusu hao masista Wakonsesioni wafuate kanuni ya Klara na kuunda monasteri nyingine, halafu Papa Julius II (1503-1513) akawapatia kanuni mpya (1511) ambayo inafanana nayo, lakini inaruhusu mali ya monasteri na kulegeza mfungo. Hata hivyo wakaachwa chini ya Ndugu Wadogo wakapewa fadhili zote za Waklara (1520). Ndiyo sababu wanaorodheshwa pamoja na Utawa II. Hao wakastawi sana Ulaya na Amerika hadi leo.
Tofauti zaidi ni Utawa wa Bikira Maria (Waanunsyata) ulioanzishwa na malkia Yoana wa Valois (+1505) kwa heshima ya Maria Mpashwa Habari. Tawi hilo halifuati kanuni ya Kifransisko, lakini toka mwanzo liko chini ya Waoservanti na linashiriki fadhili za Waklara: ndiyo sababu linaorodheshwa pamoja nao.
Katika kipindi hicho ni vigumu sana kutoa takwimu za idadi ya masista. Kati yao, mbali ya watakatifu 5 waliotajwa, walipatikana wenye heri 7.
Marekebisho kuendelea (1517-1762)
[hariri | hariri chanzo]Baada ya utengano wa Ndugu Wadogo (1517) monasteri zilizo nyingi ziliwekwa chini ya Waoservanti, hata zile za Wakoleta (nyingine tena zikaongezwa baadaye, k.mf. zile zote za Hispania na Ureno mwaka 1566). Kama kawaida mzigo huo ulilalamikiwa na mkutano mkuu (1532); hivyo ikakatazwa monasteri nyingine zisipokewe chini ya OFM pasipo ruhusa ya mkutano, na hasa wahusika washughulikie mahitaji ya kiroho tu ya Waklara. Baada ya Mtaguso wa Trento kutoa maagizo kuhusu watawa wanawake (1563) yaliyochangia marekebisho ya sheria na hasa juhudi kwa maisha magumu, mkutano mkuu wa OFM ulitunga sheria muhimu kwa utekelezaji wake ukifuta wadhifa wa ndugu msimamizi wa Waklara na kuwaweka moja kwa moja chini ya Watumishi wa kanda (1565). Lakini Waoservanti walipojaribu kusawazisha mno, kwa kudai monasteri zote ziwe na mali (ilivyoruhusiwa na Mtaguso) wakapatwa na matatizo makubwa, hasa kwa sababu Wakoleta hawakukubali kuacha ufukara mkuu, na kuja kulingana na Waurbani wenye kutegemea mali zao.
Urekebisho wa Ndugu Wadogo Wakapuchini ulisababisha mapema tawi jipya la Waklara linalodumu hadi leo. Mwanzilishi ni Maria Lorenza Llonc (+1542) mjane Mhispania aliyeishi Napoli (Italia) na kuhudumia wagonjwa pamoja na jumuia ya wanawake Wafransisko wasekulari aliyoianzisha. Wakapuchini walipohamia hospitali yake (1529), akawakabidhi uongozi wa jumuia hiyo. Kati ya 1533 na 1538 wakaongozwa na Gaetano wa Thiene aliyewaelekeza kwenye maisha ya sala tu na kuwatafutia idhini ya kuishi kimonaki kwa kufuata kanuni ya Klara (1535). Baadaye akawakabidhi tena Wakapuchini, kwa kuwa karama yao iliathiri sana monasteri hiyo na roho yake, na ndivyo alivyotaka mwanzilishi. Papa Paulo III (1534-1549) akathibitisha hayo na nia yao ya kushika kikamilifu kanuni (1538). Kwa ajili hiyo mwanzilishi aliikamilisha katiba ya Koleta kwa kutumia ile ya Wakapuchini. Sifa ya monasteri ikaenea haraka na kusababisha kabla ya 1600 zianzishwe 17 nyingine Italia (Karolo Boromeo aliunda tatu katika jimbo lake). Ila Wakapuchini wanaume wakakataa katakata kuzisimamia, isipokuwa mbili. Hata hivyo dada zao wakaendelea kuomba msaada huo kwa kuwapitia Maaskofu na wafalme, mpaka Mapapa wakalazimisha hao wanaume kuhudumia walau kiroho monasteri fulanifulani. Hata nje ya Italia wakaenea haraka: Hispania (1588), Ufaransa (1603), Ureno (1625), Mexico (1665) ambayo ikawa nchi walipoongezeka zaidi hadi leo, Peruu (1713), Gwatemala (1725), Chile (1727) n.k.
Hata marekebisho mengine ya Utawa I yalijaribu bure kukataa huduma kwa Waklara, hasa Wariformati waliojitahidi sana ili Mapapa wawaweke wote chini ya Maaskofu. Hatimaye wakalazimika kuwahudumia Waklara. Masista wa Utawa II na III waliokuwa chini ya Warekoleti wakaja kutumia jina hilo pia.
Marekebisho mengine ya Waklara yalifanyika katika karne XVII, hasa Italia. Kati yake ule wa Wakaapweke wa Mt. Petro wa Alkantara, ulioanzishwa na Kardinali Mkapuchini na kuthibitishwa na Papa Klementi X (1670-1676), ndio tawi gumu kuliko yote yaliyowahi kuwepo. Masista hao waliishi kila mmoja peke yake kama Wakartusi na kujitahidi kumuiga Petro wa Alkantara katika yote, lakini hawakuenea sana.
Katika karne XVII na XVIII hata Waurbani wakapata marekebisho yao hasa upande wa ufukara, Ufaransa na Italia.
Waklara waliorekebishwa walitoa mifano bora ya kutetea imani na ubikira wakati wa uenezi wa Uprotestanti na vita vya dini vilivyofuata. Upungufu uliosababishwa na mambo hayo Ulaya Kaskazini ulifidiwa kabisa sio tu katika nchi zilizobaki kuwa za Kikatoliki, bali hata Amerika na Asia. Wakonsesioni walifika Mexico mwaka 1540. Waklara wakafungua monasteri yao ya kwanza ya Amerika huko Hispaniola mwaka 1551. Monasteri nyingine zikaanzishwa karne hiyohiyo Peruu, Ekwado, Kolombia, Chile, Gwatemala na Brazili. Katika karne XVII Waklara wakaenea Ufilipino (1621) na China (1633). Katika karne XVIII ongezeko liliendelea ingawa kasi yake ilipungua.
Takwimu ni kama ifuatavyo: Mwaka 1587 Waklara tu walikuwa 28,000 katika monasteri 618 (Hispania + Ureno 277, Italia + visiwa 199, Ufaransa 91, Ulaya ya Kati 46, Amerika 5). Monasteri za Wakonsesioni zilikuwa 76 na za Waanunsyata 9. Mwaka 1680 Waklara tu walikuwa 38,000 katika monasteri 973 (Hispania + Ureno 394, Italia + visiwa 248, Ufaransa 182, Ulaya ya Kati 128, Amerika 21). Monasteri za Wakonsesioni zilikuwa 90 na za Waanunsyata 40. Kati yao wote anang’aa hasa Veronika Giuliani (+1727) aliyejaa karama na njozi tangu utotoni, alivyosimulia kwa utiifu na unyofu katika shajara yenye kurasa 22,000. Wako pia wenye heri 4.
Karne za mwisho (1762-2005)
[hariri | hariri chanzo]Kama ilivyowatokea Ndugu Wadogo, Waklara pia walishambuliwa na siasa mpya za serikali, kuanzia Austria na nchi zote zilizokuwa chini yake (1782-1783), monasteri zote zilipofutwa. Uamuzi huohuo ulichukuliwa Ufaransa (1792); miaka 2 baadaye Yosefina Leroux akauawa kwa kosa la kuanza tena kuishi kijumuia), halafu Ubelgiji, Italia, Ujerumani na Hispania. Katika nchi hiyo ya mwisho monasteri nyingi zikaendelea hata baada ya sheria nyingine kudai zifutwe; pengine ilitumika mbinu ya kukubali kutoa huduma fulani (k.mf. shule) Lakini katika nchi nyingine monasteri nyingi zikakoma, hasa Ureno ambapo zilikwisha zote kufuatana na sheria ya mwaka 1834.
Tangu miaka ya kwanza ya karne XIX monasteri zikaundwa tena Ufaransa na Ubelgiji, pamoja na kuanzishwa mashirika mengi ya Kifransisko. Mojawapo ni tunda la Maria Klara Bouillevaux (+1871) aliyelianzisha Paris (1854), likifuata kanuni ya Utawa Hasa III na katiba maalumu, yenye jambo la pekee la kuabudu ekaristi saa zote. Mwaka 1912 monasteri zake zote zikapokea kanuni ya Urbani IV na kujiita Waklara Fukara wa Kuabudu Mfululizo, halafu Wafransisko wa Sakramenti Kuu. Walienea sana na kudumisha uhusiano na Wakapuchini. Hata katika nchi nyingine monasteri mpya ziliundwa na nyingine zilifunguliwa tena. Baadhi ziligeuka kuwa mashirika ya kitume, bila ya kuacha kanuni ya Kiklara.
Katika karne XX uenezi ukaendelea hasa katika nchi za Amerika na za misheni. Baada ya Mkusanyo wa Sheria za Kanisa idara ya Papa kwa Watawa iliagiza itungwe katiba moja kwa Waklara wote, isipokuwa Wakapuchini. Kazi hiyo ilifanywa polepole na OFM kwa kupokea mapendekezo ya maabesi pia, ikapitishwa (1930), lakini si kwa Wakoleta. Kwa Waklara Wakapuchini katiba ilitungwa na wenzao wa kiume na kupitishwa mapema zaidi (1927). Waurbani pia wakaja kukubaliwa katiba maalumu (1973). Juhudi hizo za kuimarisha umoja zilichangiwa sana na Papa Pius XII (1939-1958) alipohimiza mashirikisho ya monasteri pamoja na kulegeza masharti ya ugo (1950) kwa lengo la kuziondoa katika hali ya ukiwa, kuzisaidia upande wa malezi na kuruhusu pengine uhamisho. Kazi hiyo ilianza Ufaransa (1953) na kuendelezwa na Mtaguso II wa Vatikani hivi kwamba mwaka 1975 kulikuwa na mashirikisho 43 (1 chini ya Wakonventuali, 7 chini ya Wakapuchini na 35 chini ya OFM). Ni mafanikio makubwa tukizingatia ugumu wa kushinda desturi za siku nyingi na tofauti za kila aina.
Uhusiano kati ya monasteri na kati ya hizo na Wafransisko wengine umeongezeka na kuinua ujuzi wa kidini na wa hali na mahitaji ya Kanisa na ya ulimwengu. Mtaguso uliagiza pia matabaka kati ya masista yafutwe; hivyo Waklara wakarudia mpango wa mwanzilishi kuhusu udugu, pamoja na kuzidi kuchimba karama yake kwa jumla. Katika uchangamfu huo mpya monasteri nyingi zikapokea kanuni I badala ya kanuni II. Hivyo mnamo mwaka 1975 kati ya monasteri za Waklara, 660 hivi zilikuwa zinafuata kanuni I na 150 hivi kanuni II. Hata sinodi ya Maaskofu kuhusu watawa (1994) ikajadili sana masuala ya wamonaki na kuhimiza tena mashirikisho yaimarishwe na ugo urekebishwe hasa kwa faida ya malezi.
Baada ya ongezeko la nusu ya kwanza ya karne XX, uhaba wa miito Ulaya umerudisha nyuma ustawi wa monasteri nyingi. Takwimu ya uenezi ni kama ifuatavyo: Mwaka 1907 Waklara tu walikuwa 11,000 katika monasteri 561 (Hispania + Ureno 185, Italia 157, Amerika 40, Ulaya ya Kati 53, Ufaransa 43). Monasteri za Wakonsesioni zilikuwa 88 na za Waanunsyata 6. Mwaka 1980 Waklara tu walikuwa 17,000 katika monasteri 824 (Hispania + Ureno 289, Italia 144, Amerika 172, Ulaya ya Kati 78, Asia+Afrika+Australia 60, Ufaransa 43). Monasteri za Wakonsesioni zilikuwa 153 na za Waanunsyata 4. Mwaka 2000 Waklara tu walikuwa 13,160 katika monasteri 926. Monasteri za Wakonsesioni zilikuwa 164 na za Waanunsyata 7. Kuhusu matawi, mwaka 2005 takwimu zilikuwa hivi: Waklara wa kawaida 7,662, Waklara Wakoleta 681, Waklara Waurbani 1,122, Waklara Wakapuchini 2,246, Wakapuchini wa Sakramenti Kuu 295, Waklara wa Kuabudu Mfululizo 587 = Jumla ya Waklara 12,593 katika monasteri 928. Wakonsesioni walikuwa 2,019 katika monasteri 157 na Waanunsyata 96 katika monasteri 8. Waklara wafiadini wengine 6 wa karne XX, hasa Wahispania, wameshatangazwa wenye heri. Mklara maarufu zaidi wa milenia mpya ni Maria Anjelika wa Kupashwa Habari ambaye, karibu na monasteri yake ya kuabudu ekaristi mfululizo, ameanzisha (1981) mtandao wa Kikatoliki mkubwa kuliko yote ya Amerika (EWTN)!
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]Orodha ya Watakatifu Wafransisko
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- The Catholic Encyclopedia: The Poor Clares
- Poor Clares Ilihifadhiwa 16 Septemba 2021 kwenye Wayback Machine. Official U.S. website
- Sala kwa ajili ya miito Ilihifadhiwa 29 Oktoba 2014 kwenye Wayback Machine.
- Konventi Mfululizo wa filamu kwa runinga