Nenda kwa yaliyomo

Abd el Kader

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Abd el Kader mnamo mwaka 1865

Abd el Kader (6 Septemba 180826 Mei 1883), (Kiarabu عبد القادر ابن محيي الدين ʿAbd al-Qādir ibn Muḥyiddīn; alijulikana pia kama Abdul Qadir, Emir Abdelkader au Abdelkader El Djezairi), alikuwa kiongozi wa kijeshi, wa kidini na wa kisiasa nchini Algeria.

Alipigana dhidi ya uvamizi wa Ufaransa katika Algeria kuanzia mwaka 1830 hadi 1847. Baada ya kushindwa aliishi Dameski na hapo aliingilia katika ghasia ya mwaka 1860 alipookoa Wakristo wengi waliotishiwa na mauaji.

Miaka ya kwanza

[hariri | hariri chanzo]

Abd el Kader alizaliwa mnamo 1807 au 1808[1] katika familia ya wataalamu wa Kiislamu walioamini walitoka katika ukoo wa mtume Muhamad[2]

Tangu utotoni alianza masomo ya dini. Alipokuwa na miaka 14 alifikia hadhi ya hafizi (mwenye kukariri kurani yote) na mwaka 1825 aliondoka kuelekea Makka kwenye safari ya hajj. Safarini aliongeza elimu yake akavutiwa na matengenezo ya Muhammad Ali Pasha aliyoyaona wakati alipopitia Misri. Alirudi Algeria miezi michache kabla ya uvamizi wa Kifaransa.

Upinzani dhidi ya uvamizi wa Kifaransa

[hariri | hariri chanzo]
Eneo la dola la Abd el Kader mnamo 1838

Miaka ya mafanikio (1830-1837)

[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1830 Algeria ilivamiwa na Ufaransa na utawala wao ulichukua nafasi iliyowahi kuwa mikononi mwa Waosmani kwa miaka 300. Wakati wa jeshi la Ufaransa kufika Oran katika Januari 1831, baba yake Abd el-Kader aliongoza majaribio ya upinzani chini ya bendera ya jihadi.

Baada ya Wafaransa kutwaa miji mikubwa wapinzani walikutana mlimani na hapo Abd el-Kader alichaguliwa kuwa kiongozi kwa cheo cha "amir". Katika muda mfupi alifaulu kuunganisha makabila ya Algeria ya magharibi chini ya uongozi wake.

Mwaka uliofuata (1834) jenerali Mfaransa Desmichels alipaswa kumtambua kama mkuu wa eneo la Oran. Patano hili liliongeza heshima yake kati ya makabila ambayo hadi hapo yalikataa kuchukua msimamo.

Chanzo cha dola

[hariri | hariri chanzo]

Hadi mwaka 1839 kulikuwa na kipindi cha amani ambapo Abd el-Kader alipanua himaya yake katika milima ya Atlas na ng'ambo hadi vyanzo vya jangwa kubwa la Sahara. Aliweka misingi ya dola lenye jeshi la kudumu na pesa yake. Mwenyewe aliishi maisha ya kawaida akikaa katika hema. Alikataa kutumia cheo cha sultani akikazia hadhi yake ya kitaalamu.

Kushindwa na kuwa mfungwa Ufaransa

[hariri | hariri chanzo]
Abd el Kader alisalimu amri (mchoro wa Kifaransa)

Kipindi cha amani kilikwisha wakati gavana mpya wa Kifaransa aliamua kupeleka walowezi katika eneo la Abd el Kader aliyewashambulia tarehe 15 Oktoba 1839. Kipindi cha vita kilifuata ambapo Wafaransa waliongeza idadi ya wanajeshi wao na kutumia mbinu kali dhidi ya makababila yaliyomsaidia Abd el Kader. Wafaransa walichoma nyumba na mazao yote wakafaulu kuvunja upinzani kwa silaha ya njaa.

Abd el Kader alivuka mpaka wa Moroko lakini Wafaransa walivamia upande ule pia. Hatimaye alilazimishwa kusalimu amri tarehe 21 Desemba 1847. Alikubali kukamatwa na na Wafaransa kwa ahadi ya kwamba watampeleka Misri. Lakini alipelekwa Ufaransa na kushikwa huko pamoja na familia yake.

Baada ya miaka 5 rais mpya wa Ufaransa Louis Napoleon Bonaparte alimweka huru, akampatia pensheni na kumruhusu kuhamia Milki ya Osmani.

Miaka ya Dameski

[hariri | hariri chanzo]
Abd el Kader jinsi alivyopokea Wakristo wa Dameski, taswira ya Jean Baptiste Huysmans ya mwaka 1861

Tangu mwaka 1852 Abd el Kader aliishi Dameski alipoendelea kutunga vitabu vya dini na falsafa.

Mwaka 1860 ugomvi uliwaka huko Lebanoni kati ya Wadruzi na Wakristo Wamaroni na mapigano yalienea hadi Dameski. Wadruzi walishambulia mitaa ya Wakristo na kuua zaidi ya watu 3,000. Hapo ni Abd el Kader aliyefungua nyumba yake kwa maelfu ya Wakristo pamoja na mabalozi Wazungu na masista Wakatoliki akaokoa uhai wao.

Kutokana na tendo hili Abd el Kader aliheshimiwa kimataifa akapokea nishani za juu kutoka Ufaransa, Ugiriki, Milki ya Osmani, Vatikani pamoja na zawadi kutoka rais Abraham Lincoln wa Marekani.

Aliaga dunia mjini Dameski tarehe 26 Mei 1883 akazikwa kando ya kaburi la msufi mashuhuri Ibn Arabi. Mabaki yake yaliondolewa kaburini mwaka 1965 na kupelekwa Algier.

  1. Wengine wanataja 6 Septemba 1808 lakini tarehe halisi haieleweki
  2. Par Société languedocienne de géographie, Université de Montpellier.

Kijisomea

[hariri | hariri chanzo]
  • Ahmed Bouyerdene, Emir Abd el-Kader: Shujaa na Mtakatifu wa Islam, trans. Gustavo Polit, Dunia Hekima 2012, ISBN 978-1936597178
  • John W. Kiser, Kamanda wa Waamini: Maisha na Nyakati za Emir Abd El-Kader, Archetype 2008, ISBN 978-1901383317
  • Elsa Marston, Huruma Warrior: Abd El-Kader wa Algeria, Hekima Hadithi 2013, ISBN 978-1937786106
  • Charles Henry Churchill, Maisha ya Abd el-Kader: Ex-Sultan wa Waarabu wa Algeria: imeandikwa na compiled kutoka yake mwenyewe dictation kutoka Vyanzo Halisi, Nabu vyombo vya Habari 2014, ISBN 978-1294672289, Reprint kutoka Chapman na Ukumbi wa 1867
  • Danziger, Raphael. Abd al-Qadir na Algerians: Upinzani dhidi ya kifaransa na Ndani ya Kuimarisha. New York: Holmes & Meier, 1977.
  • Etienne, Bruno. Abdelkader. Paris: Hachette Littérature, 2003.
  • Kiser, John W. Kamanda wa Waamini: Maisha na Nyakati za Emir Abd el-Kader (1808-1883). Rhineburg: Monkfish, 2008.
  • Jennifer Pitts, trans. na ed. Maandiko juu ya Dola na Utumwa na Alexis de Tocqueville. Baltimore: Johns Hopkins University Press, 2000.
  • Abd-el-Kader au château d'Amboise. Bordeaux: Imprimerie de H. Faye. 1849. OCLC 457413515.
  • Abd-el Kader : Sa vie intime, sa lutte avec la France, son avenir. Bordeaux: Lacaze. 1860. OCLC 493227699.
pFad - Phonifier reborn

Pfad - The Proxy pFad of © 2024 Garber Painting. All rights reserved.

Note: This service is not intended for secure transactions such as banking, social media, email, or purchasing. Use at your own risk. We assume no liability whatsoever for broken pages.


Alternative Proxies:

Alternative Proxy

pFad Proxy

pFad v3 Proxy

pFad v4 Proxy