Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatimaye WHO na wadau wafanikiwa kufika Gaza Kaskazini na kufikisha misaada

Familia zilizotawanywa na machafuko Gaza zinapokea msaada wa chakula kutoka Umoja wa Mataifa
© WFP/Ali Jadallah
Familia zilizotawanywa na machafuko Gaza zinapokea msaada wa chakula kutoka Umoja wa Mataifa

Hatimaye WHO na wadau wafanikiwa kufika Gaza Kaskazini na kufikisha misaada

Msaada wa Kibinadamu

Baada ya kukosa vibali vya kuingia eneo la Gaza Kaskazini tangu katikati ya mwezi Januari mwaka huu, hatimaye shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO limefanikiwa kuingia eneo hilo na kujionea hali ya wananchi na mahitaji ya afya yalivyo pamoja na kupeleka misaada ikiwemo vifaa vya matibabu na mafuta ya kuendeshea mitambo ya hospitali.

Mwakilishi wa WHO katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu Dkt. Rik Peeperkok ameeleza kuwa waliyoshuhudia huko Gaza kaskazini ni hali ya kutisha sana kwani baadhi ya majengo katika hospitali ya Al- Awda yamebomolewa na hospitali pekee ya watoto ya Kamal Adwan imelemewa na wagonjwa.

WHO na wadau wake wamefanikiwa kufika hospitali ya Al Shifa iliyo kaskazini na kupeleka mafuta(ya kuendeshea mitambo), baadhi ya vifaa vya kuokoa maisha kwa wagonjwa 150 na matibabu ya watoto 50 waliokuwa na utapiamlo mkali na pia kupeleka chanjo,” alisema Dkt. Rik Peeperkorn.

Kitengo cha watoto katika kituo hicho ndio kuliporipotiwa watoto 10 kufa kutokana na njaa na upungufu wa maji mwilini katika siku za hivi karibuni na “kimeelemewa na wagonjwa”, alisema Dkt. Peeperkorn.

Hali katika Hospitali ya Al-Awda ilikuwa “ya kutisha haswa”, aliendelea kueleza wakati akitoa ombi la dharura la kuhakikisha kuna ufikiaji endelevu wa misaada ya kibinadamu. “Mfumo wa kuleta utatuzi unahitaji kuendelea kufanya kazi ili misaada iweze kuwafikia wale wenye uhitaji,” alisisitiza akirejea itifaki ambapo wapiganaji wanaarifiwa mapema kuhusu maeneo ya misaada ya kibinadamu.

Vizuizi

Kwa mujibu wa Dkt. Peeperkorn, misheni nyingi za WHO kaskazini zilikataliwa mwezi Januari; ni tatu tu kati ya 16 ziliidhinishwa, nne "zilizuiliwa" na tisa "zilikataliwa". "Hakukuwa na misheni hata moja iliyofanikiwa mwezi Februari," aliwaambia waandishi wa habari huko Geneva.

Ingawa mahitaji ni makubwa zaidi kaskazini mwa Gaza, watu wengi zaidi kote katika Ukanda huu wanategemea msaada wa kibinadamu baada ya karibu miezi mitano ya vita ambavyo vimewafanya watu wapatao milioni 1.5 kuyahama makazi yao katika mkoa wa kusini wa Rafah.

Utapiamlo - ambao unasababisha unyafuzi kwa watoto wadogo - haukuwa kamwe tishio kuu la Gaza kama ilivyo sasa, kwani eneo hilo lilijitosheleza kwa samaki na uzalishaji mwingine wa chakula, Dk. Peeperkorn alisisitiza.

“Kabla ya uhasama wa miezi ya hivi karibuni, unyafuzi katika Ukanda wa Gaza ulikuwa nadra huku asilimia 0.8 tu ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano wakiwa na utapiamlo," alielezea. "Kiwango cha (sasa) cha asilimia 15.6 cha unyafuzi miongoni mwa watoto chini ya miaka miwili kaskazini mwa Gaza kinaonesha kupungua kwa kasi. Kupungua kwa hali ya lishe ya idadi ya watu katika miezi mitatu haijawahi kutokea ulimwenguni.

Afisa huyo wa WHO alibainisha kuwa na wasiwasi kwamba asilimia 90 ya watoto chini ya miaka miwili na asilimia 95 ya wanawake wajawazito na wanaonyonyesha "wanakabiliwa na umaskini mkubwa wa chakula - maana yake wamekula makundi mawili au chini ya kiwango cha chakula kinachohitajika katika siku iliyopita.” 

Chaguo la kudondosha misaada kwa njia ya angani kumepunguza bei 

Misaada ta kibinadamu inayodondoshwa kutoka hewani na ndege huko Gaza imesaidia kwa wakati huu ambao ni vigumu misaada kufikishwa kwa njia ya ardhini. Hadi kufikia sasa Umoja wa Mataifa haujashiriki katika misheni hiyo ya kudondosha misaada ilisema ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada, OCHA, hii leo na kueleza kwamba itaendelea “kuchunguza kila njia ili kuhakikisha kwamba misaada inawafikia wanaohitaji”.

“Lengo letu la wazi ni kuongeza usafiri wa nchi kavu ili ulingane na mahitaji makubwa tunayosikia," alisema msemaji wa OCHA Jens Laerke.

“Watoto wanapoanza - kama madaktari wanavyowaambia wenzetu - kufa njaa, hiyo inapaswa kuwa onyo kama hakuna jingine; kama si sasa, ni wakati gani wa kuvuta vituo, kufurika Gaza kwa msaada unaohitaji.”

Kabla ya kuongezeka kwa mzozo hivi karibuni huko Gaza, karibu lori 500 kwa siku ziliingia Gaza, lakini hesabu ya kila siku katika miezi na siku za hivi karibuni ni nadra hata kufika lori zaidi ya 133, Bwana Laerke alielezea.

“Tunaendelea kuwasiliana na mamlaka na kila mtu anayehusika ambaye anaweza kutusaidia kupata fursa hizo ili tuweze kupata misaada kwa kiwango kikubwa Lakini kwa sasa hatuna (ruhusa za kuingia).”

"Mbaya zaidi kuliko Vita ya pili ya dunia "

Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa huko Geneva hii leo lilisikia kwamba hadi asilimia 80 ya makazi katika maeneo ya kaskazini mwa Gaza sasa yameharibiwa au kubomolewa tangu mashambulizi ya Israel yalipoanza dhidi ya wanamgambo wa kipalestina wa Hamas kufuatia Hamas kuishambulia Israel Oktoba 7, 2023. 

"Yote ambayo yanafanya makazi kuwa 'ya kutotosha' - upatikanaji wa huduma, ajira au utamaduni - shule, maeneo ya kidini, vyuo vikuu, hospitali - yote yamesawazishwa," alisema Balakrishnan Rajagopal, Ripota Maalum kuhusu makazi ya kutosha. 

“Kiwango hiki na ukubwa wa uharibifu ni mbaya zaidi kuliko huko Aleppo, Mariupol au hata Dresden na Rotterdam wakati wa Vita vya Pili vya dunia.”

Mtaalamu huyo huru wa haki, ambaye si mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa, alikuwa akitoa ripoti yake kwa Baraza la haki za binadamu ambalo kikao chake cha 55 kinaendelea mjini Geneva.

pFad - Phonifier reborn

Pfad - The Proxy pFad of © 2024 Garber Painting. All rights reserved.

Note: This service is not intended for secure transactions such as banking, social media, email, or purchasing. Use at your own risk. We assume no liability whatsoever for broken pages.


Alternative Proxies:

Alternative Proxy

pFad Proxy

pFad v3 Proxy

pFad v4 Proxy