Mwaka 2024 ulighubikwa na machungu lakini kuna matumaini 2025 - Guterres
Mwaka 2024 ulighubikwa na machungu lakini kuna matumaini 2025 - Guterres
Kwa mwaka mzima wa 2024, imekuwa vigumu kupata matumaini. Vita vimesababisha maumivu makubwa, machungu na ukimbizi, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres katika ujumbe wake wa mwaka mpya, 2025 uliotolewa leo Desemba 30 jijini New York, Marekani.
Guterres amesema katika mwaka 2024, ukosefu wa usawa na mgawanyiko vinaongezeka – na kuchochea mvutano na kukosa imani, na zaidi ya yote, “na leo naweza kuripoti rasmi kuwa tumevumilia muongo wa joto kali.Miaka 10 yenye joto zaidi ni katika miaka 10 iliyopita ikiwemo 2024. Huku ni kuvurugika kwa tabianchi – mbele ya macho yetu. Lazima tuondoke kwenye mwelekeo huu wa uharibifu – na hatuna muda wa kupoteza.”
Hata hivyo Katibu Mkuu amesema mwaka 2025, nchi lazima zielekeze dunia katika njia salama kwa kupunguza kwa kiasi kikubwa hewa chafuzi na kuunga mkono mpito kuelekea mustakabali wa nishati salama.
Hata katikati ya kiza kuna matumaini
Amesema ni muhimu – na inawezekana kwani hata katika siku za kiza zaidi, ameona matumaini yakichochea mabadiliko.
“Naona matumaini kwa wanaharakati – vijana na wazee – wakipaza sauti zao kwa maendeleo. Naona matumaini kwa mashujaa wa kibinadamu wakivuka vikwazo na kusaidia watu walio hatarini zaidi. Naona matumaini kwa nchi zinazoendelea zikipambana kusaka haki ya kifedha na tabianchi,” amesema Katibu Mkuu.
Halikadhalika amesema anaona matumaini kwa wanasayanasi na wagunduzi wakichukua hatua tofauti kwa ajili ya ubinadamu.
Fursa zitokanazo na Mkataba wa Zama Zijazo
Na zaidi ya yote Aliona matumaini mapya Septemba, viongozi wa dunia walipokutana na kupitisha Mkataba wa Zama Zijazo kwani, “Mkataba ni hatua mpya ya kusongesha amani kwa kuzuia kusambaa kwa silaha. Kurekebisha mfumo wa fedha duniani ili usaidie na kuwasilisha mataifa yote.”
Guterres amesema ni hatua ya kushinikiza fursa zaidi kwa wanawake na vijana. Kushinikiza kuweka kanuni ili teknolojia iweke mbele watu na haki zaidi badala ya mchakato wa takwimu usiodhibitiwa.
Na kila mara, kuzingatia maadili na kanuni za haki za binadamu, sheria ya kimataifa na Chata ya Umoja wa Mataifa. Hakuna hakikisho la kilicho mbele ya 2025.
Amehitimisha ujumbe wake akisema “naahidi kushikamana na wale wote wanaosongesha mustakabali wenye amani zaidi, usawa, tulivu na afya kwa wote. Kwa pamoja, tunaweza kufanya 2025 kuwa mwanzo mpya. Si kama dunia iliyogawanyika. Bali mataifa yaliyoungana.."