Zaidi ya watoto 70 wameuawa Gaza tangu Januari 1 huku gharama za maisha zikizidi kupanda
Zaidi ya watoto 70 wameuawa Gaza tangu Januari 1 huku gharama za maisha zikizidi kupanda
Amani na Usalama
Hali ya maisha kwa raia wa Gaza inaendelea kuwa mbaya msimu huu wa baridi kali kutokana na vikwazo vya kufikisha misaada, kupanda kwa gharama za maisha na mashambuizi yanayoendelea kukatili maisha ya raia wakiwemo watoto 74 waliouawa tangu Januri Mosi mwaka huu yamesema mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF ambalo linasema kuuawa kwa watoto hao 74 katika siku saba za kwanza za mwezi huu ni dhihirisho la jinamizi linaloendelea kuighubika Gaza na mashambulizi ya Israel hayaonyeshi dalili yoyote ya kukoma ikiwemo ya jana usiku katika mji wa Gaza, Khan Younis na kwenye makazi ya Pwani ya wakimbizi wa ndani ya Al Mawasi ambayo Israel yenyewe iliyatenga hapo awali kama maeneo salama.
Kwa mujibu wa UNICEF jana Jumanne pekee watoto 5 wameripotiwa kuuawa Al Mawasi. Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEFF Catherine Russell amesema "Kwa watoto wa Gaza, mwaka mpya umeleta vifo zaidi na mateso kutokana na mashambulizi, kunyimwa huduma, na kuongezeka kwa hali ya baridi. Usitishaji wa mapigano umechelewa kwa muda mrefu na watoto wengi sana wameuawa au kupoteza wapendwa wao katika mwanzo mbaya wa mwaka mpya.”
Gharama za chakula zinaendelea kupanda Gaza
Kwa upande wake shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula Duniani WFP limesema kana kwamba mashambulizi hayatoshi sasa kupanda kwa gharama za chakula ni mtihani mwingine kwa watu wa Gaza kwani kilo 25 za unga zinauzwa hadi dola za Marekani 150 gharama ambayo watu wengi hawawezi kumudu na watoto ni wahanga wakubwa wakilzimika kulala njaa.
Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X limesema linapokuja suala la mashambulizi Gaza “Hakuna tofauti, wahudumu wa kibinadamu, hata wawe ni nani nao wamekuwa wakilengwa mara kwa mara. Kupuuzwa huku kwa wazi kwa sheria za kimataifa za kibinadamu hakuwezi kuachwa kuwa ndio kawaida mpya.”
Pia limesema Gaza hospitali zimekuwa mitego ya vifo, familia zimesambaratika, watoto wanakufa kwa baridi na njaa inakatisha maisha ya watu wengi