Shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA, lilianzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 8 Desemba 1949 ili kutekeleza mipango ya moja kwa moja ya misaada na kazi kwa wakimbizi wa Kipalestina, kufuatia vita vya 1948. Shirika hilo lilianza kufanya kazi tarehe 1 Mei 1950.
Mkusanyiko huu kutoka Picha za Umoja wa Mataifa unaainisha kazi muhimu ambayo shirika hilo limekuwa likifanya katika eneo hili kwa miaka 74 iliyopita.
Wakati shirika hilo la Umoja wa Mataifa lilipoanza operesheni mwaka 1950, lilikuwa likikabiliana na mahitaji ya wakimbizi wa Kipalestina wapatao 750,000. Hivi leo, takriban wakimbizi milioni 5.9 wa Kipalestina katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, Jordan, Lebanon na Syria wanastahiki kupokea huduma za UNRWA.
Picha hii iliyopigwa kwenye ufuo wa bahari karibu na Gaza, muda mfupi baada ya kuwasili kwa Kikosi cha Dharura cha Umoja wa Mataifa katika Ukanda wa Gaza, inaonyesha wakimbizi wakipakua magunia ya unga ambayo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) lilisafirisha hadi Gaza kwa meli ndogo Mei 1957.
Shirika ili hlilifanya shughuli mbali mbali. Mwaka 1954, UNRWA ilianza mradi wa kuchimba kwenye mchanga na kufanya angalau theluthi moja ya uwanda wa udongo upatikane kwa ajili ya kulimwa na wakimbizi.
Misafara ya ngamia ilileta miche kwenye eneo lililokuwa likitunzwa tena, na mwishoni mwa 1956, zaidi ya miche 2,500,000 ilikuwa imepandwa ili kulinda dunamu 3,700 za ardhi inayoweza kulimwa katika eneo la matuta ya mchanga.
UNRWA imechangia ustawi na maendeleo ya binadamu ya vizazi vinne vya wakimbizi wa Kipalestina, wanaoelezwa kama ni "watu ambao makazi yao ya kawaida yalikuwa Palestina wakati wa 1 Juni 1946 hadi 15 Mei 1948, na ambao walipoteza nyumba na njia za kujipatia riziki kama matokeo ya vita vya 1948.
Umoja wa Mataifa unasimama na wakimbizi wa Kipalestina. UNRWA inajitahidi kuhakikisha watoto waathrika wa mizozo wanaendelea na masomo licha y achangamoto nyingi. Katibu Mkuu António Guterres alipigwa picha ya pamoja na wanafunzi alipotembelea shule moja ya zamani inayoendeshwa na UNRWA.