UDADAVUZI: Maendeleo hayapaswi kuja kwa gharama ya mazingira wasema mkutano wa UN wa bayoanuwai Cali Colombia
Nchi tofauti kutoka kote ulimwenguni zimekusanyika katika jiji la Cali, Colombia,kujadili jinsi ya kulinda bayoanuwai na kuunda mpango wa kudumu wa jinsi binadamu wanavyoweza kuishi kwa amani na asili.
Zaidi ya nchi 190 zilitia sahihi Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Bayoanuwai, na wajumbe wamekusanyika nchini Colombia kwa ajili ya Mkutano wa 16 wa Umoja wa Mataifa wa Nchi Wanachama, au COP16, mkutano unaofanyika kila baada ya miaka miwili ili kukubaliana kuhusu ahadi za kulinda mazingira.
Kauli mbiu ya mkutano huo ni "Amani na Mazingira," ikitambua kwamba maendeleo ya kiuchumi hayapaswi kuja kwa gharama ya mazingira.
COP16 haipaswi kuchukuliwa kuwa sawa na mkutano wa COP29 kuhusu mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika Baku, Azerbaijan, mwezi ujao.
Mambo matano unayohitaji kujua kuhusu masuala yanayoshughulikiwa huko Cali.
Mikakati ya nchi
Kila nchi iliyotia saini mkataba imejiandaa kuendeleza mipango ya kufikia malengo mbalimbali yaliyoainishwa katika Mfumo wa Kimaataifa wa Bayoanuwai wa Kunming-Montreal, ambao ni mpango wa kimataifa ulioanzishwa katika COP15 nchini Canada.
Malengo makuu ya mkataba huu ni kulinda asilimia 30 ya sayari, ikiwa ni pamoja na maeneo ya ardhi, bahari, na maeneo yaliyo na maji safi, na kuyabadilisha kuwa maeneo ya yaliyolindwa ifikapo mwishoni mwa muongo huu.
Zaidi ya hayo, mfumo huo unasisitiza urejeshaji na ulinzi wa mifumo muhimu ya ikolojia, kama vile misitu ya mvua na maeneo oevu.
“kufikia sasa, chini ya nchi 35 pekee ndio zimewasilisha mipango yao,” anasema Juan Bello, mkurugenzi wa kanda na mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Maataifa la mazingira UNEP barani Amerika ya Kusini na Karibea
“Msingi wa mkutano huu ni kukagua malengo yaliyopendekezwa na kila nchi kwa ajili ya kutekeleza mfumo wa kimataifa ili kuona kama watafanikiwa katika lengo la kuzuia kupotea kwa bayoanuwai."
Kufadhili hatua: Dola bilioni 700 zahitajika
Kulinda bayoanuwai huja na gharama kubwa. Dola bilioni 700 zinahitajika kuanzisha hatua hiyo.
“Kwa sasa, dola bilioni 200 kwa mwaka zinahitajika,” anasema Juan Bello. Dola bilioni 500 zaidi zinahitajika katika sekta za kiuchumi kama vile chakula na nishati ili “kubadilisha ruzuku ambazo kwa sasa zinadhuru bayoanuwai.”
Mfano wa ufadhili wa kutekeleza mfumo wa kimataifa wa bayoanuwai ni muhimu kwa mafanikio yake. Hii inajumuisha chanzo cha ufadhili na jinsi kitakavyosimamiwa.
Kufuatilia maendeleo
Washiriki wanaokutanan huko Cali pia wanajadili jinsi bora ya kupima maendeleo ya nchi binafsi.
“Nchi hizi zinahitaji kukubaliana kuhusu viashiria, jinsi ya kupima na kuthibitisha, na hili ni gumu sana,” amekiri mtaalamu huyo wa UNEP.
Manufaa ya rasilimali za kiasili
Mfumo huo pia unajumuisha ahadi kuhusu matumizi endelevu ya rasilimali za asili kwa lengo la kuhakikisha kwamba manufaa yanayopatikana kutoka kwa rasilimali za kijenetiki yanashirikiwa kwa haki na usawa, hasa kwa jamii ambazo ni wahifadhi wa rasilimali hizo.
Rasilimali za kijenetiki zina maana ya nyenzo zozote za kibiolojia zinazomilikiwa na viumbe hai, ambazo zina taarifa za kijenetiki zenye thamani halisi au inayoweza kutekelezeka.
“Inatarajiwa kwamba wale wanaotumia taarifa hii kwa madhumuni ya kiviwanda, kwa mfano, katika sekta ya dawa, katika sekta ya urembo na chakula, wataweza kulipa kwa sababu ni matumizi ya kiviwanda na kibiashara,” anasema Juan Bello.
Wazo ni kwamba matumizi haya yanazalisha malipo ambayo yanaweza kufaidisha nchi na jamii ambapo bayoanuwai hii inapatikana. Hili ni suala gumu sana, lakini ni muhimu kabisa, anasema Bello.
Watu wa asili
Mkataba wa Bayoanuwai pia unatambua umuhimu wa maarifa ya jadi ya watu wa asili, na wajumbe huko Cali wanaangaziajinsi ya “kuhakikisha kwamba watu wa asili wanaweza kupata fursa ya kutambuliwa na masharti yote ili michango yao katika uhifadhi wa bayoanuwai ikubaliwe ipasavyo,” anaongeza Bello.
Jukumu la watu wa asili ya Kiafrika wanaochangia katika uhifadhi, urejeshaji, na matumizi endelevu ya bayoanuwai pia linajadiliwa.
Matarajio
Matarajio ya kuwepo kwa maendeleo yanatarajiwa katika nyanja nyingi. “Jambo muhimu sana ambalo linaweza kutoka kwenye mkutano huu ni kutambuliwa kwamba hatua za kurekebisha mifumo ya ikolojia ni za msingi katika kukabiliana na mzozo wa tabianchi,” anasema mwakilishi wa UNEP, akiongeza kuwa ni muhimu “kuunda uhusiano wa moja kwa moja, wazi na unaoleta uwiano kamili baina ya bayoanuwai na mabadiliko ya tabianchi.”