Content-Length: 103854 | pFad | http://news.un.org/sw/story/2024/12/1183051

Baada ya kunusuriwa na programu ya IOM, mhamiaji kutoka Ethiopia asema katu hatorudi Yemen - IOM | Habari za UN
Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baada ya kunusuriwa na programu ya IOM, mhamiaji kutoka Ethiopia asema katu hatorudi Yemen - IOM

Mfanyakazi wa IOM akiwasajili wahamiaji kutoka Ethiopia huko Ma'rib, Yemen, kabla ya kusafiri kwenda Addis Ababa.
© IOM Yemen/Elham Al-Oqabi
Mfanyakazi wa IOM akiwasajili wahamiaji kutoka Ethiopia huko Ma'rib, Yemen, kabla ya kusafiri kwenda Addis Ababa.

Baada ya kunusuriwa na programu ya IOM, mhamiaji kutoka Ethiopia asema katu hatorudi Yemen - IOM

Wahamiaji na Wakimbizi

Janga la kibinadamu likizidi kushika kasi nchini Yemen, shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM linaongeza kasi ya mpango wake wa kurejesha wahamiaji nyumbani kwa hiari, VHR. Mradi huu hupatia wahamiaji waliokwama njia salama ya kurejea nyumbani kwao. Kupanuliwa kwa mradi huu kunafuatia idadi ya wahamiaji nchini Yemen kuongezeka na kufikia 6,300 mwezi Oktoba mwaka huu, kwa mujibu wa mfuko wa IOM wa  Ufuatiliaji wa wahamiaji.

Mwaka huu wa 2024, IOM imeshafanya safari 30 za ndege kupitia mradi huo wa VHR ikiwemo ya tarehe 5 mwezi huu waDesemba ambapo wahamiaji 175 wa Ethiopia walirejeshwa Yemen kutoka uwanja wa ndege wa Aden. Makala hii inafuatilia miongoni mwa wahamiaji hao yaliyowasibu hadi kukubali kurejea nyumbani kwa hiari. 

Video ya shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM nchini Yemen,  inaanza vijana wanne wakiwa kwenye eneo kame, mimea inayostawi hapa ni ya jamii ya miiba tu. Umsikiaye ni Faiz, kijana raia wa Ethiopia mhamiaji hapa Yemen, taifa la kusini magharibi mwa rasi ya Arabia, ukanda wa Asia Magharibi.

Anasema alifika hapa Yemen kwa sababu ya mzozo unaoendelea nchini mwao. Hakuna fursa za ajira na hakuna chakula.

Faiz anasimulia safari ya kutoka Ethiopia hadi hapa Yemen.

Tulimlipa msafirishaji haramu riyali elfu moja za Saudia sawa na dola 266 za kimarekani. Nilifika hapa ili niweze kuelekea moja kwa moja Saudi Arabia. Lakini mpakani kuna changamoto.”

Kupitia video hii ya shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM, Faiz anaendelea kuelezea matarajio yake wakati wa safari hiyo.

“Saudi Arabia ningaliweza kufanya kazi kama mchungaji wa mifugo au mkulima kwa mwaka mmoja au miaka miwili kisha ningalirejea nyumbani.”

Wahamiaji wengi waliokwama huko Ma’rib, Yemen wanasubiri kurejea nyumbani.
© IOM/Haithm Abdulbaqi
Wahamiaji wengi waliokwama huko Ma’rib, Yemen wanasubiri kurejea nyumbani.

IOM inasema kila mwaka, wahamiaji kama Faiz hufanya safari hatari wakitafuta maisha bora. Njiani hukabiliwa na changamoto lukuki na za hatari. Hupitia mazingira magumu kupata huduma muhimu.

“Tunalala nje mitaani, tunakula mabaki ya vyakula. Na hakuna kazi Yemen. Lakini watu hapa ni wazuri sana wanajaribu kutusaidia.”

Mhamiaji mwingine kutoka Ethiopia hapa Yemen ni Alamudin. Yeye anasema, nilipata kazi ya kufanya usafi kwenye hospitali. Lakini ujira haukutosheleza mahitaji yangu. Walinilipa dola 25 kwa mwezi. Nililala kwenye ushoroba wa hospitali.Nilikula mlo mmoja kila baada ya siku moja. Kama kuna staftahi, basi hakuna mlo wa mchana. Na kama kuna mlo wa mchana basi hakuna mlo wa jioni.

Angalau Alamudin yeye ana dada yake ambaye amekuwa anaishi Saudi Arabia kwa miaka 10 sasa. Huyu amekuwa mkombozi kwa familia yao kwani hutuma fedha za kusaidia familia yao Ethiopia kuweza kujikimu.

Alamudin anasema anafanya kazi ya usafi. Anatuma fedha nyumbani.

Kilio cha wahamiaji kama Faiz na Alamudin kikafikia IOM nchini Yemen ambayo ikaelekeza usaidizi wa aina tofauti tofauti. Mathalani kuwawezesha kupata huduma muhimu kupitia mradi uitwao Migrants Response Points (MRP) ambao huwawezesha kupata huduma za ulinzi, afya, msaada wa kisaikolojia na pia afya ya akili.

Msaada mwingine ni kuwawezesha kurejea nyumbani kwa hiari, au VHR.

“Nilikuwa natembea kuelekea Aden, mji ulioko Yemen, ndipo gari la IOM likasimama. Waliniita na kunipeleka kwenye mradi wa MRP wa usaidizi wa huduma kwa wahamiaji.  Huko walinisajili. Mke wangu aliondoka kurejea Ethiopia kwa ndege ya mwisho Nashukuru Mungu kwamba hapa tunapata maji, chakula, nguo na mahali pa kulala. Na kisha wataturudisha nyumbani Ethiopia kwa ndege.”

Video inaonesha wahamiaji akiwemo Faiz wakiwa na virago vyao wakielekea kupanda ndege, ambapo IOM inasema mradi wa kurejesha wahamiaji nyumbani kwa hiari ni mpango muhimu kwa wahamiaji waliokwama ambao ndoto zao za kwenda maeneo kama Saudi Arabia zimeishia Yemen ambako hali si hali. Faiz anatamatisha akisema..

“Sitorudi tena hapa. Kazi yangu hapa imekwisha.”









ApplySandwichStrip

pFad - (p)hone/(F)rame/(a)nonymizer/(d)eclutterfier!      Saves Data!


--- a PPN by Garber Painting Akron. With Image Size Reduction included!

Fetched URL: http://news.un.org/sw/story/2024/12/1183051

Alternative Proxies:

Alternative Proxy

pFad Proxy

pFad v3 Proxy

pFad v4 Proxy