Content-Length: 105521 | pFad | http://news.un.org/sw/story/2024/12/1183321

FAO Tanzania yatoa mafunzo ya ufugaji wa nyuki kupitia Mradi wa ACP MEAs 3 | Habari za UN
Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO Tanzania yatoa mafunzo ya ufugaji wa nyuki kupitia Mradi wa ACP MEAs 3

FAO Tanzania yatoa mafunzo ya ufugaji wa nyuki kupitia Mradi wa ACP MEAs 3.
FAO Tanzania
FAO Tanzania yatoa mafunzo ya ufugaji wa nyuki kupitia Mradi wa ACP MEAs 3.

FAO Tanzania yatoa mafunzo ya ufugaji wa nyuki kupitia Mradi wa ACP MEAs 3

Tabianchi na mazingira

Mradi wa ACP MEAs 3 unaoendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO, na kufadhiliwa na Muungano wa Ulaya, EU umetoa mafunzo ya ufugaji nyuki kwa wakulima nchini Tanzania. Mradi huu unawapa wakulima zana na ujuzi muhimu katika ufugaji nyuki endelevu, na hivyo kuboresha maisha yao huku wakikuza bayoanuwai na uhifadhi wa mazingira. Kwa kuunga mkono jamii za wenyeji, Mradi huu unalenga kukuza ukuaji wa uchumi na kuwawezesha wakulima kulinda wachavushaji, ambao ni muhimu kwa uzalishaji katika kilimo na afya ya mfumo ikolojia.

Kupitia video iliyoandaliwa na FAO Tanzania Diana Mahimbali, Afisa wa ufugaji nyuki katika wilaya ya Kilosa iliyoko mkoani Mororgoro  Mashariki mwa Tanzania, anasema mradi wa ACP MEAs3 umebadilisha maisha yao "Tumepokea mafunzo ya ufugaji nyuki yenye lengo la kuongeza thamani ya mazao ya nyuki kwa sababu tunaamini kwamba uongezaji wa thamani kwa bidhaa unaanza shambani."

FAO Tanzania yatoa mafunzo ya ufugaji wa nyuki kupitia Mradi wa ACP MEAs 3, na kuwapatia wakulima vifaa vya ufugaji nyuki.
FAO Tanzania
FAO Tanzania yatoa mafunzo ya ufugaji wa nyuki kupitia Mradi wa ACP MEAs 3, na kuwapatia wakulima vifaa vya ufugaji nyuki.

Mafunzo ya ufugaji nyuki na matumizi mazuri ya viuatilifu yanayotolewa na mradi huo, yanalenga kuwapatia washiriki ujuzi na maarifa muhimu ili kuondokana na vitisho na changamoto za siku zijazo sambamba na kulinda bayoanuai.

Amani kamagi ni mwalimu katika wilaya ya Kilolo mkoani humo. Ni mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ya ufugaji nyuki, anasema "Kupitia mafunzo haya, nimejifunza kuwa nyuki ni muhimu sana kwa maisha yetu ya kila siku na ni wadudu rafiki kwa sababu wanaongeza uzalishaji wa chakula."

Mbali ya mafunzo mradi huu wa FAO pia unawapatia wafugaji nyuki stadi za mchakato na usindikaji wa asali. Rubia Aroni ni mfugaji nyuki katika wilaya ya Kilosa, hapa akiwa anachuja asali na kuimimina kwenye chupa kwa ajili ya kuhifadhi na kuuza anaeleza ni nini ametoka nacho "Kutoka kwenye mafunzo ya ufugaji nyuki, nilipenda suala la kuchuja asali. Pia, kuna vitu vingi tofauti katika usindikaji wa asali ambavyo sikuvijua hapo awali. Lakini nimejifunza kupitia mafunzo ya leo. Nashukuru sana FAO kwa mafunzo hayo"

FAO Tanzania yatoa mafunzo ya ufugaji wa nyuki kupitia Mradi wa ACP MEAs 3. Nelson Mbigo, ni mkulima  kutoka wilaya ya kilosa na mnufaika wa mafunzo hayo.
FAO Tanzania
FAO Tanzania yatoa mafunzo ya ufugaji wa nyuki kupitia Mradi wa ACP MEAs 3. Nelson Mbigo, ni mkulima kutoka wilaya ya kilosa na mnufaika wa mafunzo hayo.

Nelson Mbigo, naye ni mkulima  kutoka wilaya ya kilosa kwa mafunzo aliyopata anatoa , shukrani akisema"Tunashukuru sana kwa mafunzo ya leo. Tumepewa vifaa maalum. kwa mfano kifaa hiki cha moshi, huku ukirina asali unatumia moshi kwani huwezi kuua nyuki kwa moshi. Tofauti na zamani tulipokuwa tunaua nyuki wengi kwa sababu hatukuwa na vifaa hivyo.”

Mradi huu wa FAO ambao unatoa mafunzo kwa wakulima wa nyuki 300 katika wilaya sita nchini Tanzania umekuwa mkombozi mkubwa kwanza umeongeza idadi ya nyuki na pili  uzalishaji wa asali na hivyo kuinua kipato cha wakulima na kuwapa ujasiri kama anavyosema Zaina Mohamed ambaye pia ni mkulima kutoka wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam "Kwa vifaa vilivyotolewa hatupaswi kuogopa nyuki. Badala yake vifaa hivi vinapaswa kutuwezesha kufuga nyuki ili tupate kujikwamua na kuendelea kimaisha.”

Soundcloud








ApplySandwichStrip

pFad - (p)hone/(F)rame/(a)nonymizer/(d)eclutterfier!      Saves Data!


--- a PPN by Garber Painting Akron. With Image Size Reduction included!

Fetched URL: http://news.un.org/sw/story/2024/12/1183321

Alternative Proxies:

Alternative Proxy

pFad Proxy

pFad v3 Proxy

pFad v4 Proxy