Syria: Harakati za usaidizi zaendelea, UNDP yafikisha nishati ya mafuta Aleppo
Syria: Harakati za usaidizi zaendelea, UNDP yafikisha nishati ya mafuta Aleppo
Katika harakati za kurejesha huduma za afya nchini Syria baada ya miaka 14 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosambaratisha huduma hizo kwa wananchi, hii leo shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo duniani, UNDP limefikisha nishati ya mafuta kwenye hospitali ya Zahi Azraq mjini Aleppo kaskazini mwa nchi.
Kupitia ukurasa wake wa X, zamani Twitter, UNDP imesema hatua hiyo ni ya dharura ili kuhakikisha hospitali hiyo inaendelea kutoa huduma muhimu kwa wale wanaohitaji.
Video iliyochapishwa kwenye ukurasa huo inamuonesha Mohamad Jasser, Afisa wa UNDP kwenye mji huo wa Aleppo ambao ni mji mkuu wa jimbo la Aleppo akisema “leo UNDP inasaidia kusongesha utendaji kazi wa hospitali ya Zahi Azraq kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza kuwa kuleta nishati ya mafuta. Hili ni jawabu la muda tu ili kuhakikisha hospitali inaweza kuendelea kutoa huduma kwa wale wanaohitaji.”
Bwana Jasser amesema tangu mwaka jana wa 2023, hospitali hiyo ambayo imekarabatiwa na UNDP imetoa huduma za afya kwa zaidi ya watu 250,000 waliokuwa wanahitaji.
“Tunatumaini kuona hili likiendelea leo,” ametamatisha Bwana Jasser.
Hatuwezi kuitelekeza Syria - IOM
Mapema jana Alhamisi, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, Amy Pope aliyewasili Damascus Syria tarehe 16 mwezi huu alisema kwa kushirikiana na wadau, wanaangalia jinsi ya kupanua wigo wa usaidizi wa kibinadamu kwa Syria nzima, lengo likiwa ni kusaidia serikali kufanikisha utulivu baada ya kuanguka kwa utawala wa Bashar Al-Assad.
“Wakati huu hatuwezi kuiacha Syria, wakati ambao ni wa matumaini makubwa na vile vile changamoto kubwa,” amesema Bi. Pope katika taarifa ya IOM iliyotolewa mjini Damascus.
Amesema kuwa IOM imejizatiti kushikamana na wasyria kushughulikia mahitaji ya sasa na ya muda mrefu na kuwasaidia kwenye njia ya kuelekea kujikwamua na kupata amani na kudumu.”
Ombi jipya la fedha la IOM n idola milioni 30 za kimarekani itakazotumia kwa miezi minne ijayo kusaidia watu 684,100 walioathiriwa na utawala ulioondolewa madarakani huko Kaskazini-Magharibi mwa Syria.
Fedha zitalenga msaada wa haraka na endelevu kwa makundi yaliyo hatarini miongoni mwa wale waliolazimika kuhama, pamoja na waliohama sasa hivi na wale wanaorejea.
Mchakato wa kisiasa Syria usiengue haki za watoto - UNICEF
Naye Mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF Ukanda wa Masharikiya Kati na Afrika Kaskazini Edouard Beigbeder amesema watoto wa Syria baada ya miaka 14 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe hakuna wanachofahamu zaidi ya vita, hali iliyowalazimu kukua mapema bila hata kufurahia utoto wao.
“Hata hivyo kuna matumaini na fursa ya mustakabali bora.” Amesema Mkurugenzi huyo kupitia taarifa ya UNICEF.
Amesema UNICEF itaendelea kusalia Syria kusaidia watoto na familia zao wanapojipanga na mwelekeo mpya wa taifa lao.
Hivyo amesema “mchakato halali na jumuishi wa kisiasa lazima upatie kipaumbele haki za watoto milioni 10 wa Syria. Kiwango cha mahitaij yao ni kikubwa kwani watoto milioni 7.5 wanahitaji misaada ya kibinadamu. Watoto milioni 6.4 wana mahitaji ya dharura ya huduma za ulinzi kwani ukosefu wa usalama na hali ngumu ya uchumi imetwamisha haki zao na kuwatumbukiza kwenye msongo.”