Content-Length: 99393 | pFad | http://news.un.org/sw/story/2024/12/1183371

Syria: Tutangulize ulinzi kwa manusura na pia kuhifadhi ushahidi wa uhalifu | Habari za UN
Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Syria: Tutangulize ulinzi kwa manusura na pia kuhifadhi ushahidi wa uhalifu

Wavulana wawili wanacheza katika kituo cha mapokezi katika mji wa Raqqa kaskazini mwa Syria. Familia zao zilirejea nchini humo hivi majuzi.
© UNICEF/Muhannad Aldhaher
Wavulana wawili wanacheza katika kituo cha mapokezi katika mji wa Raqqa kaskazini mwa Syria. Familia zao zilirejea nchini humo hivi majuzi.

Syria: Tutangulize ulinzi kwa manusura na pia kuhifadhi ushahidi wa uhalifu

Amani na Usalama

Siku kumi na moja tangu kukoma kwa utawala wa kiimla uliodumu kwa miongo mitano nchini Syria, viongozi wa ngazi mbalimbali za Umoja wa Mataifa wamendelea kusisitiza hitaji la kutanguliza ulinzi wa manusura na uhifadhi wa ushahidi wa uhalifu.

Tunakutana na mama mmoja akisema maelfu ya Wasyria wamepitia kwa takribani miaka Hamsini ya utawala wa familia ya Bashar al-Assad tangu enzi za utawala wa baba yake, Hafez al Hassad aliyeitawala Syria tangu mwaka 1971 hadi mwaka 2000.

Katika kituo cha afya cha Al Tamayoz jijini Damascus, Mama huyu, jina limehifadhiwa, katika mazungumzo na Mkuu wa ofisi ya  Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Dharura, OCHA Tom Fletcher anasema mume wake aliwekwa kizuizini. Baada ya mwaka mmoja wa kukaa kizuizini, walimpa hati zilizosema kwamba mume wake amefariki dunia.

Wakati mapinduzi ya hivi karibu ambapo kundi la Hay’at Tahrir al-Sham (HTS)  lilipotwaa mamlaka katika mji Mkuu Damascus yakileta matumaini na nafasi ya amani na utulivu, lakini bado Umoja wa Mataifa unaona kwamba Wasyria wanahitaji usaidizi iwe ndani ya nchi yao na hata kwingineko walikokimbilia kutokana na hali ya awali n ahata ya sasa. Mathalani hivi karibuni Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, Rema Jamous Imseis akizungumza na wanahabari jijini Geneva, Uswisi alisema,

"Ni muhimu kukumbuka kuwa watu hawa wanarejea katika nchi ambayo imeharibiwa na miaka 14 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Tuna zaidi ya Wasyria milioni 7 waliokimbia makazi yao nchini humo, na zaidi ya asilimia 90 ya watu wanaishi chini ya mstari wa umaskini na wanategemea aina fulani ya usaidizi wa kibinadamu ili kuendelea kuishi. Kwa hivyo wakati tunatumai kuwa maendeleo ya sasa yatamaliza shida hii, inabidi pia tutambue kuwa mabadiliko katika serikali haimaanishi kuwa tayari kuna mwisho wa janga la kibinadamu. Wasyria ndani ya nchi na nje ya nchi bado wanahitaji ulinzi na msaada."

Pia juzi tarehe 17, katika ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Geneva, Uswisi, Mkuu wa Mfumo wa Kimataifa, Usio na Upendeleo na wa Kujitegemea wa Kuchunguza Uhalifu Mzito nchini Syria (IIIM), Robert Petit, aliwaambia waandishi wa habari kwamba, "sasa kuna uwezekano wa kupata ushahidi wa kuhusika katika uhalifu kwa mamlaka za juu na washirika wao. Pia kuna uwezekano wa hatimaye kutafuta hatima ya makumi ya maelfu ya Wasyria ambao walikamatwa kinyume cha sheria na kuwekwa kizuizini."

Naye Hanny Megally, Kamishna wa Tume Huru ya Kimataifa ya Uchunguzi kuhusu Syria, wakati wa mahojiano na Idhaa ya Umoja wa Mataifa, anasisitiza haja ya kutanguliza ulinzi wa manusura na uhifadhi wa Ushahidi akisema,

"Ni idadi kubwa ya kazi mbele ya mamlaka mpya, lakini kimsingi tunaanza na juhudi za kusema, tuanze kwa kuwalinda wale ambao wamenusurika na hili, na tuangalie kulinda ushahidi ili kuweza kuwasaidia kujua ukweli na kuwawajibisha wale ambao wanahusika zaidi.”

Na je, ana maoni gani kuhusu kwamba bado baadhi ya mataifa duniani yameiwekea vikwazo Syria hata wakati huu ambao imepata utawala mpya?

"Kinachoweza kufanya kazi hivi sasa ni kusimamishwa kwa muda kwa vikwazo. Inaruhusu nchi kuanza kupata msaada kutoka nje. Nchi Wanachama zinaweza kuhukumu ikiwa mambo yanakwenda katika mwelekeo sahihi na hiyo inaweza kuimarishwa.”









ApplySandwichStrip

pFad - (p)hone/(F)rame/(a)nonymizer/(d)eclutterfier!      Saves Data!


--- a PPN by Garber Painting Akron. With Image Size Reduction included!

Fetched URL: http://news.un.org/sw/story/2024/12/1183371

Alternative Proxies:

Alternative Proxy

pFad Proxy

pFad v3 Proxy

pFad v4 Proxy