Maburg: Rwanda yatangaza mwisho wa mlipuko, WHO yapongeza
Maburg: Rwanda yatangaza mwisho wa mlipuko, WHO yapongeza
Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) limeipongeza serikali ya Rwanda kwa kufanikiwa kuudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Maburg. Hii leo Rwanda imetangaza mwisho wa mlipuko wa hivi karibuni wa ugonjwa huo baada ya kutokuwepo maambukizi mapya katika siku 42 na mgonjwa wa mwisho akiwa amepimwa mara mbili bila kukutwa na ugonjwa kama matakwa ya WHO yanavyotaka ili kutangaza kuisha kwa mlipuko wa magonjwa namna hii.
Huyo ni Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moet akisema, "hii ni hatua muhimu kwa serikali na watu wa Rwanda na kwa watu wa kanda ya Afrika na ulimwengu. Ningependa kupongeza serikali ya Rwanda na jamii ambazo zilikuwa sehemu ya mwitikio huu kwa matokeo mazuri dhidi ya mlipuko wa ugonjwa”.
Mlipuko huo wa Maburg uliothibitishwa tarehe 27 Septemba mwaka huu 2024, ulikuwa mlipuko wa kwanza wa Ugonjwa wa Virusi vya Marburg nchini Rwanda. Jumla ya watu 66 walikutwa na ugonjwa huo na vifo 15 vilirekodiwa. Takriban asilimia 80 ya maambukizi hayo yalikuwa miongoni mwa wahudumu wa afya walioambukizwa walipokuwa wakitoa huduma za kimatibabu kwa wenzao na kwa wagonjwa wengine.
Kutumwa kwa wataalam wa WHO, timu ya wataalamu kutoka nchi zingine katika kanda na uhamasishaji mkubwa wa juhudi za kitaifa za serikali ya Rwanda zilikuwa muhimu katika kuimarisha hatua dhidi ya ugonjwa huo.
Mkuu wa WHO kanda ya Afrika, hapa anatoa ahadi kwamba WHO itaendelea kufuatilia ili kuhakikisha kwamba maambukizi yoyote yatakayojitokeza yanagundulika haraka. Pia anasema bila shaka wataendelea kuiunga mkono serikali ya Rwanda katika kuwahudumia ambao wameathirika.
Virusi vinavyosababisha Marburg, viko katika familia moja na virusi vinavyosababisha Ugonjwa wa Ebola. Ni hatari sana na kiwango cha vifo ni kuanzia asilimia 24 hadi 88. Katika mlipuko huu wa sasa, kiwango cha vifo kilikuwa cha chini karibu asilimia 23. Virusi vya Marburg huwafikia watu kutoka kwa wanyama popo-walao matunda na huenea kati ya wanadamu kwa kugusana moja kwa moja na majimaji ya mwili kutoka kwa watu walioambukizwa, au hata katika maeneo mengine ambako majimaji hayo yamegusa.