Content-Length: 102113 | pFad | http://news.un.org/sw/story/2024/12/1183491

Kilimo kwenye mstari wa mbele katika hatua za dharura DRC | Habari za UN
Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kilimo kwenye mstari wa mbele katika hatua za dharura DRC

FAO inafanya kazi na jamii kuanzisha vikundi vya majadiliano na vitendo vinavyoitwa Vilabu vya Dimitra, maeneo salama na jumuishi ambapo wanawake na wanaume wa vijijini hupata suluhu kwa masuala ya jumuiya.
© FAO/Andrea Sanchez Enciso
FAO inafanya kazi na jamii kuanzisha vikundi vya majadiliano na vitendo vinavyoitwa Vilabu vya Dimitra, maeneo salama na jumuishi ambapo wanawake na wanaume wa vijijini hupata suluhu kwa masuala ya jumuiya.

Kilimo kwenye mstari wa mbele katika hatua za dharura DRC

Wahamiaji na Wakimbizi

Sasa, wanaishi hapa katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Rusayo 2 ili kuepuka mzozo unaoendelea katika eneo hilo na kujilinda wao na watoto wao, wakitumai siku moja kuanza maisha mapya.

Rusayo 2 kwa sasa  imejaa, na kuwalazimisha watu wapya waliowasili kuishi maeneo ya pembezoni mwa kambi. Msongamano huu sio tu unasumbua rasilimali chache za kambi lakini pia unaweka watu zaidi katika hatari za kiusalama, kwani wakazi wanasalia katika hatari ya kushambuliwa na vikundi vilivyojihami.
 
Hatari ya uhaba wa chakula inazidi kuwa mbaya kadiri kambi inavyokua. Ukweli huu si vigumu kwa mtu yeyote wa nje kuuona, hasa kwa wataalam kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO).
 
"Hali katika maeneo mengi inatisha sana katika suala la uwezo wa watu kupata huduma za msingi zaidi, iwe ni usafi wa mazingira au makazi. Kambi ya wakimbi wa ndani  ya Rusayo 2 tayari imejaa, na watu 30,000 wa ziada wanakuja na hakuna nafasi ya kutosha ya kuwahudumia. Hali ya uhakika wa chakula ni mbaya sana hapa – hasa kwa wapya waliowasili, lakini pia kwa wakazi wa muda mrefu,” anasema Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Beth Bechdol, katika ziara yake ya Rusayo 2.
 
DRC inakabiliwa na janga la muda mrefu wa kibinadamu, unaochochewa na mzozo wa matumizi ya silaha unaoendelea na hali mbaya ya hewa ya mara kwa mara, na kusababisha wakimbizi wengi wa ndani na kusukuma mamilioni kwenye ukingo wa njaa.
 
Katika kipindi cha kati ya Januari na Julai 2024, mzozo ulilazimisha zaidi ya watu milioni 1.4 kuondoka makwao. Kwa ujumla, kambi zinahifadhi wakimbizi wa ndani milioni saba, asilimia 89 wakiwa katika majimbo ya mashariki.
 
Kwa upande wa uhaba wa chakula, maeneo mengi ya wakimbizi wa ndani yameainishwa katika Ngazi ya Dharura [Ainisho ya Awamu Jumuishi ya Uhakika wa Chakula (IPC) Ngazi ya 4], ikimaanisha kuwa watu wanakabiliwa na viwango vikubwa vya uhaba wa chakula, na mapungufu makubwa kati ya wakati wanakula na wakati wasipokula, na viwango vya juu vya utapiamlo. Kwa sehemu ya kwanza ya 2025, makadirio yanaonesha uwezekano wa kutokea hali kama hiyo.
 
Kutokana na hali kuwa mbaya zaidi, FAO imetoa ombi la dola milioni 330 kwa mwaka ujao kwa ajili ya afua za dharura za kilimo na mnepo.
 
"Kilimo cha dharura ni njia ya gharama nafuu, yenye matokeo kusaidia walio hatarini zaidi nchini DRC. Lakini tunahitaji kusonga mbele zaidi ya kufanya tu mwitikio wa kibinadamu kuwa na ufanisi zaidi na kutumia afua za kilimo pia ili kuongeza mnepo dhidi ya majanga yajayo,” anasema Rein Paulsen, Mkurugenzi wa FAO wa Dharura na Mnepo.
 
Bechdol, Paulsen na Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa FAO na Mwakilishi wa Kanda ya Afrika, Abebe Haile-Gabriel, walitembelea kambi ya Rusayo 2 na maeneo mengine ya mradi wa FAO ili kutathmini mahitaji ya msingi na kuamua masuluhisho ya kuongeza mwitikio wa FAO.
 
Kwa sasa, FAO inazisaidia kaya 25,000 zilizo katika mazingira magumu, au takriban watu 150,000, katika Kivu Kaskazini na Ituri, ikiwa ni pamoja na kambi ya Rusayo, kupitia vocha za fedha zisizo na masharti, kilimo cha bustani ndogo na pembejeo za uzalishaji wa mifugo. Msaada huu unawezesha IDPs kukidhi chakula chao cha haraka na mahitaji mengine ya kimsingi.
 

Hata hivyo, kuna mengi zaidi yake

 
"Katika kambi hii, FAO haitegemei tu kupatikana kwa haki za msingi za binadamu ikiwa ni pamoja na haki ya chakula, lakini pia inalenga katika kujenga uwezo wa mnepo kwa kaya zilizo hatarini zaidi. Kuona vipengele hivi muhimu - mtazamo huu wa pande mbili - katika miradi ya FAO imekuwa ya kutia moyo sana. Kwa upande mmoja, unaona haja kubwa na kwa upande mwingine, unaona matumaini, baadhi ya msisimko na shauku fulani kutoka kwa kambi, kutoka kwa wakazi, kutoka kwa wakimbizi wa ndani wenyewe," Bechdol anasema.
 
Kwa hakika, vifaa vya kilimo vidogo vya FAO vimesaidia familia, hata kwenye mita chache tu za mraba za ardhi, kukuza mbogamboga, ikiwa ni pamoja na biringanya, nyanya, kabichi, njugu, spinachi na mchicha.
 
"Tulitembelea maeneo ya wakimbizi wa ndani na kuona matokeo ya kuokoa maisha ya bustani ndogo na afua zinazohusiana ambazo zinatoa chakula chenye lishe katikati ya maeneo haya ya IDP," anasema Paulsen.
 
Familia nyingi pia huunganisha bustani ndogo na ufugaji wa sungura na kuku, kwa kutumia taka kutoka kwa wanyama kurutubisha udongo na kuongeza tija.
Mbegu bora za mbogamboga na wanyama wadogo zinazotolewa na FAO zinahakikisha kuwa watu wanapata lishe bora kila siku na pia kupata mapato kwa kuuza bidhaa za wanyama pamoja na mazao ya kilimo.
 
Akitembelea nyumba ya Riziki Ange, mama wa watoto kumi wanaoishi katika kambi ya wakimbizi wa ndani, Bechdol anaelezea, “Si kwamba muda mrefu uliopita alipokea idadi ndogo tu ya sungura kutoka FAO. Ilikuwa dume mmoja na jike watatu ambao sasa wamekuwa sungura 32.”
 
"Alifurahishwa sana na msaada huo mdogo ili kumfanya aanze na kupanua shughuli zake. Unaweza kusema kwamba alikuwa amekaribia kuwa mjasiriamali kwa jinsi alivyokuwa akijishughulisha na shughuli hii,” Bechdol anasimulia.
 

Uwezeshaji wa wanawake wa vijijini

 
Upande mwingine wa Ziwa Kivu, huko Bukavu, mamia ya wanawake hukusanyika pamoja kama sehemu ya Vilabu vya Dimitra kujadili changamoto za ndani na njia za kuzikabili. Vilabu vya Dimitra ni mpango muhimu unaoungwa mkono na FAO ambao unawawezesha wakazi wa vijijini, hasa wanawake na vijana, kuanzisha mageuzi ya kijamii, kimazingira na kiuchumi katika jamii zao.
 
Kwa wanachama wa klabu, FAO iliandaa mfululizo wa mafunzo juu ya kuongeza tija ya kilimo kupitia mbinu za kilimo endelevu.  Wanawake hao pia walipata mbegu bora na usaidizi wa ufugaji wa mifugo ili kuzalisha chakula zaidi, hivyo kuwawezesha kuuza ziada sokoni kwa nia ya siku moja kuanzisha biashara zao.
 
 








ApplySandwichStrip

pFad - (p)hone/(F)rame/(a)nonymizer/(d)eclutterfier!      Saves Data!


--- a PPN by Garber Painting Akron. With Image Size Reduction included!

Fetched URL: http://news.un.org/sw/story/2024/12/1183491

Alternative Proxies:

Alternative Proxy

pFad Proxy

pFad v3 Proxy

pFad v4 Proxy