Baraza Kuu la UN lapitisha bajeti ya UN ya dola bilioni 3.72 kwa mwaka 2025
Baraza Kuu la UN lapitisha bajeti ya UN ya dola bilioni 3.72 kwa mwaka 2025
- Ni ya kuanzia Januari 1 hadi Desemba 31 2025
- Ni ongezeko la dola milioni 1 zaidi ya pendekezo la bajeti lililowasilishwa na Guterres
- Baraza limepitisha pia mpango wa muongo mzima kusaidia nchi zinazoendelea zisizo na bahari
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha bajeti ya dola bilioni 3.72 kwa ajili ya matumizi ya Umoja huo kwa mwaka ujao wa 2025 na vile vile kupitisha mpango mpya wa usaidizi kwa nchi zinazoendelea zisizo na bahari, LLDCs.
Hatua hiyo ya Jumanne wiki hii imeashirika kukamilika kwa sehemu kuu ya majukumu ya mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ulioanza mwezi Septemba mwaka huu na utamalizika mwezi Septemba mwakani.
Bajeti ni ongezeko la dola milioni 1 zaidi ya ombi la Katibu Mkuu
Bajeti hiyo ya dola bilioni 3.72 ya matumizi ya kawaida kwa mwaka 2025 ni ongezeko kwa dola milioni 1 zaidi ya pendekezo la bajeti lililowasilishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa mwezi Oktoba mwaka huu mbele ya Kamati ya Tano ya Baraza Kuu ambayo inahusika na masuala ya utawala na bajeti.
Halikadhalika inajumuisha marekebisho ya kiufundi kufuatia kupitishwa kwa maazimio mengine ya Umoja wa Mataifa na maamuzi mengine ya taasisi za Umoja wa Mataifa tangu kuwasilishwa kwa mapendekezo ya bajeti. Bajeti nzima kwa mwaka 2025 ni dola 3,717,379,600.
Bajeti hii ya kawaida inatumika kwenye programu za Umoja wa Mataifa kwenye maeneo ya kimsingi kama vile, masuala ya kisiasa, Haki na sheria, ushirikiano wa kikanda na maendeleo, haki za binadamu, masuala ya kibinadamu na taarifa kwa umma.
Vile vile, Umoja wa Matiafa una bajeti mahsusi kwa ajili ya operesheni za ulinz iwa amani, ambayo mwaka wake wa fedha ni Julai 1 hadi Juni 30, ilhali mwaka wa fedha wa Umoja wa Mataifa kwa bajeti ya kawaida Januari 1 hadi Desemba 31.
Mpango wa Utekelezaji kwa LLDCs 2024-2034
Katika hatua nyingine, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha Programu ya Utekelezaij kwa nchi zinazoendelea zisizo na bahari kwa muongo wa 2024-2034, ikilenga kutatua changamoto za kipekee zinazokabili mataifa hayo yasiyo na bahari.
Nchi zisizo na bahari au LLDCs, zinakabiliwa na vikwazo vya biashara na maendeleo, zikitegemea nchi zingine kupitisha bidhaa zao, jambo linalosababisha gharama kubwa za biashara, kuchelewa kwa bidhaa na kupungua kwa ushindani kwenye soko la kimataifa.
Programu hii ya Utekelezaji inaainisha maeneo matano: Kuendeleza ukuaji uchumi endelevu kupitia ugunduzi na marekebisho ya mifumo, kuimarisha ujumuishaji wa biashara kikanda, kuimarisha muunganiko kwenye usafirishaji, kujenga mnepo kwa tabianchi, na kuhakikisha utekelezaji fanisi wa mikakati.
Mfumo huo mpya unaendeleza Programu ya Utekelezaji ya Vienna (2014-2024) na the Programu ya Utekelezaji ya Almaty (2003), ambayo imejenga msingi wa kutatua changamoto lukuki zinazotwamisha LLDCs.