Syria: Damascus yaangukia mikononi mwa wapinzani UN yaahidi kuendelea kusaidia kadri iwezavyo
Syria: Damascus yaangukia mikononi mwa wapinzani UN yaahidi kuendelea kusaidia kadri iwezavyo
Jinamizi la giza la vita limeacha madhara makubwa kwa watu wa Syria ambao wamevumilia karibu miaka 14 ya mateso yasiyokoma na hasara isiyoelezeka, "lakini leo kwa tahadhari tunatazamia kwa matumaini kufungua ukurasa mpya, sura ya amani, upatanisho, utu na kujumuishwa kwa Wasyria wote," amesema Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Syria Geir Pedersen baada ya taarifa zinazotoka Syria kusema sasa mji mkuu Damascus umeangukia mikononi mwa vikosi vya upinzani vya Hayat Tahrir al-Sham (HTS).
Katika taarifa yake iliyotolewa leo Bwana. Pedersen amerejelea kusisitiza mshikimano wake na watu wote waliokumbwa na madhila hayo akisema “Wakati chi inaashiria inapitia wakati wa machafuko katika historia yake mateso, ya kifo, uharibifu, watu kuwekwa kizuizini na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ninashikamana na watu hao."
Kauli ya mjumbe huyo maalum imekuja “baada ya habari kwamba mji mkuu Damascus alfajiri yaleo ulianguka mikononi mwa wapinzani wa Syria baada ya kutwaa maeneo makubwa ya nchi katika muda wa siku chache na habari kwamba Rais Bashar al-Assad anaachia ngazi na kuondoka nchini humo.”
Wakati wa matarajio mapya kwa wakimbizi wa Syria
Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa wakati huu unaweka upya matarajio ya waliokimbia makazi yao kurejea katika makazi yao waliyopoteza, na ni mwanzo wa kuunganishwa kwa familia zilizotenganishwa na vita.
"Kwa wale waliowekwa kizuizini isivyo haki, na kwa familia za wafungwa na watu waliopotea, kufunguliwa kwa milango ya gereza kunatukumbusha ni kwa kiasi gani hatinaye haki inatendeka," amesema.
Huku akionya kwamba “Changamoto kubwa bado zinaendelea amesema tunawasikia wale ambao wana hofu na wasiwasi, ni wakati wa kukumbatia uwezekano wa kufungua ukurasa mpya na kwamba ujasiri wa watu wa Syria unatoa njia ya kuelekea Syria yenye umoja na amani."
Kwa ajili hiyo, Mjumbe huyo Maalum “amesisitiza dhamira ya wazi iliyoonyeshwa na mamilioni ya Wasyria kwa ajili ya mipango thabiti na shirikishi ya mpito, kwa taasisi za Syria kuendelea kufanya kazi, na kuwawezesha watu wa Syria kuanza kuandaa mkondo huo ili kukidhi matakwa yao halali, na. kuirejesha Syria iliyoungana katika mamlaka yake, uhuru na uadilifu, kwa njia ambayo inaweza kuamrisha uungwaji mkono na ushiriki wa jumuiya nzima ya kimataifa."
Amesema Wasyria wengi, yakiwemo makundi yenye silaha na mashirika ya kiraia, wamemweleza katika taarifa hadharani nia yao ya kuwalinda ndugu zao wa Syria na taasisi za serikali katika siku zijazo dhidi ya kisasi na madhara.
Wito kwa Wasyria wote
Katika muktadha huu, Pedersen “ametoa wito wa wazi na usio na shaka kwa wahusika wote wenye silaha chini humo kudumisha tabia njema, sheria na utulivu, kulinda raia na kuhifadhi taasisi za umma."
Pia amewataka “Wasyria wote kutoa kipaumbele katika mazungumzo, umoja na kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu wanapojaribu kujenga upya jamii yao.”
Alisisitiza haja ya juhudi za pamoja ili kuhakikisha amani na utu kwa wote, pia utayari wake wa kuwaunga mkono watu wa Syria "katika safari yao ya kuelekea mustakabali thabiti unaojumuisha watu wote na kuamuliwa na kutengenezwa na watu wa Syria."
Amesema "Tuheshimu kumbukumbu ya wale ambao wameteseka kwa miongo kadhaa kwa kujitolea kusaidia Wasyria kujenga Syria ambapo haki, uhuru na ustawi ni hali halisi. Tusimame kwa mshikamano na Wasyria ili kuwasaidia kuhakikisha kuwa sura hii mpya ni sura ya matumaini na fursa kwa kila Msyria."
Mwisho wa miongo ya mfumo wa ukandamizaji: Tume ya uchunguzi
Paulo Sérgio Pinheiro, mkuu wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya Uchunguzi kuhusu Syria, amesema watu wa Syria wanapaswa kuruhusiwa kuutazama wakati huu wa kihistoria "kama mwisho wa miongo kadhaa ya ukandamizaji wa serikali." Ameongeza kuwa "Kuachiliwa kwa wafungwa baada ya miongo kadhaa ya kuzuiliwa kiholela kutoka kwa gereza maarufu la Sednaya nje ya Damascus ni jambo ambalo mamilioni ya Wasyria hawakuweza kufikiria siku chache zilizopita. Hivyo sasa ni wajibu wa maafisa waliopo kuhakikisha kwamba uhalifu huo hautokei tena asilani katika kuta za Sednaya au katika kituo kingine chochote cha magereza Syria.”
Katika taarifa iliyotolewa leo, tume hiyo imebainisha kuwa kuachiliwa kwa maelfu ya wafungwa ambao wameteseka kwa miaka, au hata miongo kadhaa, ya kizuizini bila mawasiliano "kutaleta unafuu mkubwa kwa watu walioachiliwa na familia zao na kutoa matumaini kwa wale ambao bado wanasubiri habari za makumi ya maelfu ya wapendwa wao waliotoweka."
Mjumbe wa tume Lynn Welchman amesema kwamba katika muda wote wa vita, "familia zilikuwa katika hatari kubwa na kulipa kiasi kikubwa cha rushwa kwa maafisa wa serikali mafisadi ili kubadilishana na habari za wapendwa wao waliozuiliwa. Sasa, katika video ambazo zimetoka hivi karibuni kutoka ndani ya vituo vya kizuizini, tunaona vyumba vilivyo na safu za rafu zilizojazwa mafaili hayo. Tahrir al-Sham na vikundi vingine vyenye silaha ambavyo sasa vinadhibiti vituo vya kizuizini vinapaswa kuwa waangalifu sana kutotawanya ushahidi wa unyanyasaji na uhalifu."
Tume imetoa wito kwa pande zote nchini Syria kuwezesha fursa ya ufikiaji wa nchi kwa watendaji huru wa kibinadamu na haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na vituo vya kizuizini.
Alisema kauli za awali za upinzani na uongozi wa serikali, zikionyesha dhamira yao ya kudumisha hulka njema na kulinda raia, zilikuwa za kutia moyo, akisisitiza kwamba matendo yao "lazima sasa yalingane na maneno yao."
Tume itatoa ripoti mpya katika siku zijazo inayoangazia uporaji mkubwa na uharibifu wa kimfumo wa nyumba ambao umeenea nchini Syria, mara nyingi kufuatia mabadiliko ya udhibiti na ufurushwaji wa watu.