Content-Length: 102455 | pFad | http://news.un.org/sw/story/2024/11/1181801

Esneda asema haogopi vitisho kutetea eneo la jamii ya asili ya Yukpa | Habari za UN
Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Esneda asema haogopi vitisho kutetea eneo la jamii ya asili ya Yukpa

Esneda Saveedra, kiongozi wa jamii ya asili ya Yukpa nchini Colombia.
UNHCR
Esneda Saveedra, kiongozi wa jamii ya asili ya Yukpa nchini Colombia.

Esneda asema haogopi vitisho kutetea eneo la jamii ya asili ya Yukpa

Tabianchi na mazingira

Jamii ya asili ya Yukpa nchini Colombia imevumilia miongo kadhaa ya migogoro na watu kutawanywa inayosababishwa sio tu na mabadiliko ya tabianchi mila kandamizi bali pia kupotea kwa viumbe hai na hivyo kutishia maisha yao. 

Esneda Saveedra ni kiongozi wa jamii hao,  akizungumza katika msitu ya ardhi yao na kando ya mto Maracas, anasistiza kuwa "hana hofu ya kutetea ardhi hii."

Ardhi anayozungumzia ni eneo hilo la mto Maracas anayotetea dhidi ya vitisho kutoka kwa waharibifu wa mazingira kufuatia yale yaliyojadiliwa katika mkutano wa 16 wa nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa wa bayonuai, COP16 uliomalizika Ijumaa iliyopita huko mjini Cali nchini Colombia. Anaongeza kuwa "Yale niliyopitia kama mtoto, changamoto zote hizo, yalinipa nguvu, yalinipa ujasiri, na yakaondoa hofu yangu."

Video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR inatupatia taswira ya juu ya eneo la makazi ya jamii ya Yukpa, msitu mnene na kisha kwenye mto Maracas, shughuli zinaendelea, wengine wakiogelea, wengine wakivua samaki, mama mmoja akisafisha kuku aliyemaliza kumchuna.

Esneda anaeleza umuhimu wa mto huu kwa maisha ya jamii yake na anaendelea kujitahidi ili kulinda mazingira hayo.

"Huu ni mto Maracas, ambapo watu wetu, mababu zangu, walivua samaki kwa ajili ya chakula kila siku. Waliharibu mazingira kwa kukata miti yote, na matokeo yake, mto ulianza kukauka. Leo, mto Maracas hauna mtiririko wa maji kama ulivyokuwa zaidi ya miaka 20 iliyopita."

Esneda na familia yake kutoka jamii ya Yukpa Colombia.
UNHCR
Esneda na familia yake kutoka jamii ya Yukpa Colombia.

Katika juhudi zake, Esneda ameanzisha mazungumzo na maafisa wa serikali katika manispaa ya Becerril, akijaribu kuleta mabadiliko na uelewa juu ya umuhimu wa kuhifadhi ardhi na utamaduni wa watu wa Yukpa.

"Kumekuwa na uratibu, kazi ya pamoja, na jambo muhimu zaidi kwangu kama mwanamke wa Yukpa imekuwa kuleta ufahamu kuhusu watu wa Yukpa na ardhi yetu. Mabadiliko ya tabianchi yametufikisha kwenye tatizo kubwa zaidi, ambalo ni upotevu wa mazao na ukosefu wa chakula. Leo hatuna chakula cha kutosha katika jamii zetu. Tunaendelea kupambana, lakini pia tuko hapa kusaidia dunia nzima kuendelea kupambana na kulinda mazingira, ardhi, na hewa. Na kusema: 'Tupo hapa kuchangia kwa ajili ya ubinadamu, kwa ulimwengu mzima.’"

Harakati zake zimekumbwa na vitisho. Anasema “Walinitishia hapa kwa kuzungumza, na kwa kusema ukweli. Mama yangu alikuwa kiongozi thabiti—na bado ni kiongozi thabiti. Na nilipokuwa mdogo, nilimsindikiza kwenye michakato yake yote ya harakati, mipango na uongozi. Niliendeleza njia hiyo ya uongozi kwa sababu niliona ni muhimu. Ilikuwa ni wajibu wangu. Nilijiambia, ‘mimi ni mwanamke ambaye nimezaliwa kutetea eneo hili.”

Kwa Esneda, kulinda ardhi ya Yukpa ni zaidi ya wajibu; ni dhamira ya kuhifadhi urithi wa mababu zake. Katika changamoto za kila siku, Esneda anabaki imara kwa matumaini kuwa jamii yake na mchango wao katika kuhifadhi mazingira utatambuliwa ulimwenguni.









ApplySandwichStrip

pFad - (p)hone/(F)rame/(a)nonymizer/(d)eclutterfier!      Saves Data!


--- a PPN by Garber Painting Akron. With Image Size Reduction included!

Fetched URL: http://news.un.org/sw/story/2024/11/1181801

Alternative Proxies:

Alternative Proxy

pFad Proxy

pFad v3 Proxy

pFad v4 Proxy