Mambo 5 unayohitaji kufahamu kuhusu usafirishaji haramu wa wahamiaji
Mambo 5 unayohitaji kufahamu kuhusu usafirishaji haramu wa wahamiaji
Usafirishaji haramu wa wahamiaji ni uhalifu unaofanywa ili kupata faida, unaoendeshwa na hitaji la kuvuka mipaka nje ya njia za kawaida na kuathiri nchi nyingi kote kote duniani.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa na Uhalifu UNODC Watu wengi husafirishwa kwa njia ya magendo ndani au katika maeneo mbalimbali, huku wengine wakisafirishwa kwa njia ya haramu katika mabara yote.
Licha ya kuongezeka kwa umakini wa kisiasa na juhudi za kimataifa za kupambana na uhalifu huu, usafirishaji haramu wa wahamiaji unaendelea kufanywa katika njia mbalimbali za kupitia ardhini, baharini na angani kote duniani, katika hali zingine bila kuadhibiwa. Hapa kuna mambo matano muhimu kuhusu usafirishaji haramu wa wahamiaji ili kukusaidia kuelewa uhalifu huu vyema.
1: Usafirishaji haramu wa wahamiaji ni biashara hatari
Mwaka 2023 ulidhihirishwa kuwa mwaka mbaya zaidi kuwahi kurekodiwa kwa watu wanaohama. Takriban watu 8,600 walipoteza maisha kwenye njia zisizo za kawaida za uhamiaji duniani, kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM kukiwa na ongezeko kubwa la asilimia 20 katika mwaka mmoja tu.
Wengi wa watu hawa walikuwa walengwa wa usafirishaji haramu wa wahamiaji. Utafiti wa hivi karibuni wa UNODC unaonyesha kwamba mtiririko wa fedha kutokana na biashara ya magendo ya wahamiaji mara nyingi huvuka mipaka, ikihusisha malipo ya magendo na uhamiaji miongoni mwa wanachama wa vikundi vya wasafirishaji haramu, na pia katika muktadha wa utakatishaji fedha wa mapato ya magendo.
Njia mbaya zaidi ya usafirishaji haramu wa wahamiaji ni kwa njia ya bahari. Takriban asilimia 60 ya vifo vinatokana na kuzama kwenye njia za baharini.
Nyingi za safari hizi za baharini hupangwa na wasafirishaji haramu. Njia za Bahari ya Mediterania ni kati ya hatari zaidi kwa wahamiaji na wakimbizi.
Cha kusikitisha ni kwamba, makumi ya maelfu ya watu wametoweka au kupoteza maisha katika eneo hili katika kipindi cha muongo mmoja uliopita. Wengi wanaokabidhi maisha yao kwa wasafirishaji haramu wanakabiliwa na matokeo mabaya, wakisafiri kwa meli zisizo faa kusafiri majini au zilizojaa kupita kiasi.
2. Usafirishaji haramu wa wahamiaji ni wa kimataifa
Usafirishaji haramu unahusisha kuwapa mhamiaji au wakimbizi usaidizi wa kuvuka mpaka wa kimataifa bila kibali kinachostahili, ili malipo yawe yamefanyika. Unaweza kufanywa kwa njia ya anga, kwa kawaida kuwezeshwa na hati ghushi au zilizopatikana kwa njia ya ulaghai, katika safari hatari za nchi kavu kupitia barabara, jangwa, misitu, milima na mito au kwenye njia ya hatari ya baharini.
Njia kuu za magendo ya nchi kavu na baharini ni pamoja na njia za Kiafrika kwa nchi kavu kuelekea Kaskazini na Kusini mwa Afrika, kwa baharini hadi nchi za Ghuba na kusini mwa Ulaya, na njia kutoka Asia ya Kusini na Mashariki ya Kati kuelekea Ulaya.
Njia haramu za nchi kavu na baharini pia huongoza kutoka Kusini na Kusini-Mashariki mwa Asia hadi nchi tajiri zaidi za Kusini-Mashariki mwa Asia na Pasifiki.
IOM inasema njia za ardhini pia zinafanya kazi kupitia Amerika ya Kusini, na kati ya Amerika ya Kusini na Amerika Kaskazini.
Usafirishaji haramu kwa njia ya anga mara nyingi huhusisha safari za ndege baina ya mabara hadi kwenye viwanja vya ndege, kabla ya kuvuka kwenda kwenye eneo la mwisho lililokusudiwa, kukiwa na vipengele vya ulaghai wa hati.
3. Usafirishaji haramu wa wahamiaji ni uhalifu wa faida
Usafirishaji haramu wa wahamiaji unakadiriwa kuwa tasnia ya uhalifu yenye faida kubwa, yambayo ina thamani ya soko la angalau dola bilioni 5.5-7.
Wasafirishaji haramu huchukua fursa ya wahamiaji na wakimbizi kwa kutumia tamaa yao ya kutaka kuhama na ukosefu wa chaguzi za kusafiri mara kwa mara ili kupata nyenzo za magendo au faida za kifedha kutoka kwao na mara nyingi hutoza ada za huduma zao za ulaghai.
Kwa kawaida hutoza usafiri, malazi, vibali vya kufanya kazi vya ulaghai, hati za kusafiria na visa. UNODC imegundua kuwa mitandao ya uhalifu kwa kawaida hutumia njia za malipo na uhamisho, kama vile pesa taslimu, ambazo ni vigumu kwa mamlaka kufuatilia.
Katika baadhi ya matukio, fedha haramu zinaibiwa na kufichwa kama mapato halali ya biashara halali, kama vile mashirika ya usafiri na uajiri wa wafanyikazi, na kisha kuchakatwa na kuhamishwa pamoja na fedha hali za kisheria.
Kwa kuzingatia hali ya siri ya biashara haramu ya wahamiaji, kufuatilia pesa ni muhimu ili kupambana na vitendo hivi vya uhalifu.
4. Usafirishaji haramu wa wahamiaji mara nyingi hauadhibiwi
Usafirishaji haramu wa wahamiaji ni uhalifu unaoweza kuzalisha faida kubwa na una hatari ndogo ya adhabu kwa wahalifu wanaohusika, hasa kwa wale walio katika ngazi za juu za mitandao ya uhalifu.
Waanzilishi wa shughuli hizi kwa kawaida hawahusiki kimwili katika kusafirisha watu kuvuka mipaka, na hivyo kuwafanya kuwa na uwezekano mdogo sana wa kutambuliwa na mamlaka. Badala yake, ni "wahusika wa kiwango cha chini wanaoonekana zaidi ambao wana hatari ya kukamatwa na kufunguliwa mashtaka.”
Kuna matukio ambapo wahamiaji na wakimbizi ambao hawawezi kuwalipa wasafirishaji haramu wanalazimishwa kuingia kwenye boti za na kuziendesha au kuchukua majukumu mengine kama malipo ya kusafirishwa.
Mkakati huu unahakikisha wahamiaji na wakimbizi watabeba dhamana ya wasafirishaji haramu ikiwa watatekwa na kukamatwa na askari wa udhibiti wa mpaka au walinzi wa pwani, na hivyo kuruhusu vikundi vya uhalifu kufanya kazi bila hatari kwa watu waliowabeba na rasilimali zao.
5. Wahamiaji wanweza kukatiliwa hata kama waliafiki kusafirishwa
Wahamiaji wanaweza kukatiliwa hata kama wahamiaji na wakimbizi hao wanaweza kuanza safari yao kwa kukubali kusafirishwa kwenda nchi fulani, wanaweza kulaghaiwa, kulazimishwa au kushurutishwa kuingia katika hali ya kufanyiwa ukatilii na wasafirishaji haramu baadaye katika mchakato huo.
Hatari ni kubwa hasa kwa wale waliokwama kwa muda mrefu na wanaohitaji kupata pesa ili kufadhili hatua inayofuata katika safari yao na kulipia usafiri wao.
Wahamiaji na wakimbizi wanaotumia mitandao haramu kukimbia nchi zao za asili au kupata fursa bora zaidi wanaweza kufanyiwa vitendo mbalimbali vya ukatili, vikiwemo biashara haramu ya binadamu, unyanyasaji, ghasia, mateso, ubakaji, kunyimwa uhuru, utekaji nyara au unyang'anyi wanapokuwa kwenye usafiri au uhamishoni.
Wanawake na wasichana mara kwa mara wanakabiliwa na unyanyasaji, ukatili wa kijinsia na ukatili wa kingono.
Kazi kubwa inayofanywa na UNODC
UNODC inajitahidi kuongeza uelewa wa pamoja na msingi wa ushahidi wa uhalifu huu, kujitahidi kupunguza hali ya ukwepaji sheria, kushughulikia hali ya kifedha ya uhalifu na kuheshimu haki za watu wanaosafirishwa kwa njia haramu.
Ofisi hiyo inasaidia nchi kuzuia usafirishaji haramu wa wahamiaji, kutoa haki na kulinda maisha na haki za binadamu kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Uhalifuwa kupangwa wa Kimataifa na Itifaki yake dhidi ya Usafirishaji haramu wa wahamiaji.
Kazi ya UNODC inachangia katika kuwalinda watu dhidi ya unyanyasaji, kutelekezwa, ukatili au hata kifo ambacho kinaweza kuhusishwa na biashara haramu ya wahamiaji.