Siku ya Kimataifa ya Wahamiaji tujikumbushe changamoto wanazokumbana nazo – António Guterres
Siku ya Kimataifa ya Wahamiaji tujikumbushe changamoto wanazokumbana nazo – António Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ujumbe wake mahususi kwa ajili ya Siku ya Kimataifa ya Wahamiaji ametoa wito kwa ulimwengu kuitumia siku hii kujikumbusha kwamba pamoja na kwamba tunasherehekea michango ambayo mamilioni ya wahamiaji hutoa kwa jamii, uchumi na nchi kote ulimwenguni lakini leo pia ni siku ya kujikumbusha changamoto ambazo wahamiaji wanaweza kukumbana nazo kuanzia kwenye chuki na ubaguzi, hadi unyanyasaji wa moja kwa moja na kubaguliwa, hadi ukatili usiofikirika wa biashara haramu ya binadamu.
Nalo Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji (IOM), leo limetangaza ombi la dola bilioni 8.2 za kimarekani kukuza uhamaji wa kawaida ulio salama na utaratibu.
Mkurugenzi Mkuu wa IOM Amy Pope, kupitia ujumbe wake kwa ajili ya leo, Siku ya Kimataifa ya Wahamiaji akiguzungumzia ombi hilo la ufadhili anasema, "ufadhili huu muhimu utasaidia programu za IOM katika zaidi ya nchi 170, kwa lengo la kufikia zaidi ya watu milioni 101."
Anaongeza kueleza kwamba Kazi ya IOM itaendelea kuzingatia malengo yao matatu muhimu ya kimkakati akiyataja kuwa ni: Kuokoa maisha na kulinda watu wanaohama. Suluhu za ufurushwaji. Na kusaidia njia za uhamaji salama, wa kawaida na ulio na utaratibu.