Content-Length: 101019 | pFad | http://news.un.org/sw/story/2024/12/1183411

Korea kasikazini inafanya kila iwezalo kupanua wigo wa nyuklia: UN | Habari za UN
Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Korea kasikazini inafanya kila iwezalo kupanua wigo wa nyuklia: UN

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kisiasa Rosemary DiCarlo akihutubia Baraza la Usalama kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea (DPRK).
UN Photo/Manuel Elías
Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kisiasa Rosemary DiCarlo akihutubia Baraza la Usalama kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea (DPRK).

Korea kasikazini inafanya kila iwezalo kupanua wigo wa nyuklia: UN

Amani na Usalama

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kisiasa Rosemary DiCarlo leo ameliambia Baraza la Usalama kwamba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea (DPRK) inajitajidi kufanya kila liwezekanalo kupanua wigo wa uwezo wake wa kijeshi wa urushaji wa makombora, mpango wa nyuklia na ushirikiano wa kijeshi na Urusi.

Ameongeza kuwa "DPRK inafanya kazi kikamilifu kupanua uwezo wake wa kijeshi kama sehemu ya mpango wa maendeleo ya kijeshi wa miaka mitano uliowasilishwa Januari 2021.”

Mwaka huu wa 2024, DPRK ilizindua kombora moja la masafa marefu ICBM, makombora manne ya masafa ya kati na makombora kadhaa ya masafa mafupi, na pia ilijaribu kurusha satelaiti ya upelelezi wa kijeshi.

Kwa mujibu wa Bi. DiCarlobaadhi ya uzinduzi huo ulihusiana na majaribio ya "vichwa vya kuongozwa na hypersonic na makombora ya vichwa vingi vya vita."

Ameangazia pia kombora la Hwasong-19, ambalo lilizinduliwa kwa mara ya kwanza Oktoba 31 na kuwa kitovu cha maonesho ya hivi karibuni ya silaha huko Pyongyang.

"Kombora hili limeweka rekodi mpya za muda wa kukimbia na mwinuko wa kurusha kuliko makombora yoyote ya ICBM ya Korea Kaskazini," DiCarlo ameongeza.

Uzalishaji wa uranium na mitambo ya nyuklia

Vifaa vya nyuklia na uzalishaji wa Uranium pia ameugusia katika maendeleo ya mpango wa nyuklia wa DPRK.

Amesema "Mwezi Septemba mwaka huu, vyombo vya habari vya serikali ya DPRK viliripoti juu ya ukaguzi wa kiongozi wa nchi kwenye msingi wa uzalishaji wa uranium. Hii inathibitisha ripoti za awali za kuwepo kwa kiwanda cha pili cha kurutubisha uranium, ambacho bado hakijatangazwa huko Kansong pamoja na kituo cha Yongbyon."

Mkurugenzi mkuu wa shirika la kimataifa la nishati ya atomiki (IAEA), amesema, kinu cha megawati 5 huko Yongbyon kilikuwa hakifanyi kazi katikati ya Agosti na katikati ya Oktoba.

Hivyo amesema "Kipindi hicho kulingana na wataalam wa IAEA, kinaweza kutumika kujaza kinu na kuanza mzunguko wake wa  saba wa uendeshaji, Uendelezaji wa mipango ya nyuklia na makombora ya DPRK vinadhoofisha upunguzaji wa kimataifa wa silaha za nyuklia na kutozienezalimesisistiza shirika la IAEA.

DiCarlo pia ameangazia ushirikiano na Urusi na ripoti za "kuongezeka kwa ushirikiano wa kijeshi kati ya DPRK na Urusi.”

“Kulingana na ripoti za vyombo vya habari, tangu 2023, DPRK imehamisha zaidi ya kontena elfu 13 zilizo na risasi, makombora na mizinga kwenda Shirikisho la Urusi," DiCarlo amesema.

Kwa mujibu wake hizi ni pamoja na bunduki za kujiendesha zenyewe za mm 170 na mifumo ya roketi nyingi ya mm 240.

Wanajeshi wa Urusi wameripotiwa kutumia makombora ya masafa mafupi yaliyotengenezwa na DPRK kuishambulia Ukraine.

Msemaji huyo wa Umoja wa Mataifa pia ameripoti kuwa zaidi ya wanajeshi 10,000 wa Korea Kaskazini wametumwa nchini Urusi, ambako walikuwa wakipewa mafunzo na vifaa.

Amesisitiza kuwa "Kulingana na taarifa rasmi za Marekani na Ukraine, wanajeshi hawa wametumwa katika eneo la Kursk nchini Urusi na wanashiriki katika mapigano kwa upande wa wanajeshi wa Urusi".

Wajibu na maazimio ya kimataifa

DiCarlo amekumbusha kuwa "maingiliano ya kimataifa na DPRK yanaamuliwa na maazimio ya Baraza la Usalama."

Alisisitiza kuwa maazimio haya yanawabana kisheria nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.

Amesema "Uhusiano wowote kati ya nchi na DPRK lazima ufanyike kwa kuzingatia vikwazo vya Baraza la Usalama. Kwa mujibu wa maazimio haya, DPRK lazima iache kusafirisha aina zote za silaha na nyenzo zinazohusiana, na nchi zote wanachama zinalazimika kuzuia ununuzi wao kutoka DPRK na raia wake”.

Wito wa diplomasia

DiCarlo ametoa wito wa kufanywa upya kwa juhudi za kidiplomasia akisema "Ushirikiano wa kidiplomasia unasalia kuwa njia pekee ya amani endelevu na uondoaji kamili wa nyuklia wa Peninsula ya Korea. Tuna wasiwasi mkubwa juu ya mvutano unaoongezeka kwenye Rasi ya Korea, ambao una madhara makubwa ya kimataifa," amesema.

Amehitimisha kwa kusema kwamba "Baraza linahitaji kuchukua hatua madhubuti kushikilia msiamamo na kanuni za kimataifa za serikali kutoeneza silaha."









ApplySandwichStrip

pFad - (p)hone/(F)rame/(a)nonymizer/(d)eclutterfier!      Saves Data!


--- a PPN by Garber Painting Akron. With Image Size Reduction included!

Fetched URL: http://news.un.org/sw/story/2024/12/1183411

Alternative Proxies:

Alternative Proxy

pFad Proxy

pFad v3 Proxy

pFad v4 Proxy