Content-Length: 102238 | pFad | http://news.un.org/sw/story/2024/12/1183426

Wasichana wakipewa fursa hakuna mchezo utakaowashinda: Mkimbizi Saido Noor | Habari za UN
Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wasichana wakipewa fursa hakuna mchezo utakaowashinda: Mkimbizi Saido Noor

Saido Omar Noor, binti mwanariadha wa mchezo wa mpira wa kikapu mwenye umri wa miaka 25 mkimbizi kutoka Somalia anayeishi Kakuma nchini Kenya.
UNHCR
Saido Omar Noor, binti mwanariadha wa mchezo wa mpira wa kikapu mwenye umri wa miaka 25 mkimbizi kutoka Somalia anayeishi Kakuma nchini Kenya.

Wasichana wakipewa fursa hakuna mchezo utakaowashinda: Mkimbizi Saido Noor

Wahamiaji na Wakimbizi

Kutana na Saido Omar Noor, binti mwenye umri wa miaka 25 mkimbizi kutoka Somalia anayeishi Kakuma kambi kubwa zaidi ya wakimbizi nchini Kenya. Kupitia video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR anasema katika jamii yake ni yeye mwanamke pekee wa Kisomali anayecheza mpira kwa kikapu au basketball.

Lakini nini kilimsukuma Saido kuamua kukiuka mila na desturi na kucheza mpira wa kikapu? Saido anasema“Nataka kuonyesha  wasichana wengine ambao wana hamasa katika jamii kwamba kama Saido amefanya basi nami naweza kufanya pia. Na pia nataka kuwa ni sauti kwa ajili yao ili waweze kufanya chochote wanachotaka.”

Saido anatumia mpira wa kikapu kuchagiza jamii yake kuachana na mila na desturi potofu kwamba kuna vitu ambavyo mtoto wa kike au mwanamke hawezi kufanya na hii anasema inaleta changamoto nyingi kwa wasichana kwenye jamii yake “Wasichana wakimbizi hapa Kakuna wanakabiliwa na changamoto nyingi, na changamoto hizi ni kama ndoa za utotoni, kukatiza masomo katika umri mdogo, lakini pia wakimaliza masomo ya juu ya sekondari, hawajui nini cha kufanya au hawana kinachowahamasisha kuwa kile wanachotaka kuwa”

Katika jamii yake Saido anachopigia chepuo ni ujumuishwaji na uwezeshwaji kupitia michezo hussan kwa wasichana wakimbizi kwani anasema“Fursa ya kushiriki michezo kwa jamii ya wakimbizi ni muhimu sana haswa kwa wasichana sababu michezo ina uwezekano mkubwa wa kubadili maisha yao.”

Saido Noor na wachezaji wenzake wakicheza Mpira wa Kikapu katika makazi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya.
UNHCR
Saido Noor na wachezaji wenzake wakicheza Mpira wa Kikapu katika makazi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya.

Akiwa mazoezini Saido anasisitiza kwamba “Michezo ni kila kitu kwetu , ni njia moja ya kujieleza , ni njia pia ya kupata fursa nje ya kambi. Na endapo ningekuwa nimepewa fursa au rasilimali zinazohitajika za mimi kushiriki mashindano ya olimpiki, ningependa kushiriki olimpiki siku moja hata mara moja. “

Na ndoto hizo si zake peke yake “Tuna vijana wengi ambao wana vipaji mbalimbali, na tuna uwezo wa kuwa huko kama wakimbizi na tunahitaji kupewa fursa sawa kama wanamichezo wengine wowote"

Thomas Bach Rais wa kamati ya kimataifa ya Olimpiki IOC aliyezuru hivi karibuni Kakuma na mkuu wa UNHCR Filippo Grandi anasema Kakuma ni moja ya kambi wanazozitupia jicho la karibu hasa katika kuunda timu ya olimpiki ya wakimbizi ambayo inaendelea kukua na kujumuisha wakimbizi kutoka kambini hapo. Sasa wameunda wakfu maalum wa olimpiki kwa ajili ya wakimbizi  na lengo ni kuhakikisha ujumuishwaji mbao kwa kiasi fulani ulizaliwa Kakuma na sasa umekuwa wa kimataifa.

UNHCR inasema michezo ina nguvu kubwa ya kushamirisha jamii, kuunda fursa, na kutoa ulinzi kwa vijana wakimbizi katika makambi na duniani kote.









ApplySandwichStrip

pFad - (p)hone/(F)rame/(a)nonymizer/(d)eclutterfier!      Saves Data!


--- a PPN by Garber Painting Akron. With Image Size Reduction included!

Fetched URL: http://news.un.org/sw/story/2024/12/1183426

Alternative Proxies:

Alternative Proxy

pFad Proxy

pFad v3 Proxy

pFad v4 Proxy