Tuwapatie wasyria kile wanachotarajia baada ya utulivu kuanza kurejea - IOM
Tuwapatie wasyria kile wanachotarajia baada ya utulivu kuanza kurejea - IOM
"Wasyria wanastahili kupata kile wanachotarajia wakirejea nyumbani, kama vile usalama, misaada na utulivu,” amesema Amy Pope, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi baada ya kumaliza ziara yake katika taifa hilo la Mashariki ya Kati.
Bi. Pope alifika Damascus, mji mkuu wa Syria tarehe 16 kufuatia kuanguka kwa utawala wa Bashar Al-Assad tarehe 8 mwezi huu wa Desemba.
“Nimeona taifa lililo njiapanda – watu wake wameazimia kusonga mbele, kujenga tena upya maisha yao huku kukiwa na sintofahamu kubwa ya mustakabali wao,” amesema Mkuu huyo wa IOM.
Takwimu zinaonesha kiza: zaidi ya wasyria milioni 16 wanahitaij msaada wa kibinadamu, huku milioni 7.2 wamefurushwa makwao sasa wakimbizi wa ndani na zaidi ya milioni 6 wanasaka ukimbizi nje ya nchi.
Changamoto ni lukuki mathalani kujumuishwa tena kwenye jamii, kupata haki kutokana na machungu waliyopitia, na kujenga upya miundombinu muhimu kama vile hospitali na shule.
Jumuiya ya kimataifa na wajibu wa kunusuru Syria
Hivyo amesema jumuiya ya kimataifa inakabiliwa na wakati muhimu wa kupatia Syria misaada muhimu inayohitajika ili kusaidia kujenga upya taifa hilo baada ya vita vya miaka 14 vilivyosambaratisha sio tu maisha ya binadamu bali pia mbinu zao za kujipatia kipato na kukuza uchumi. “Tuweke pia njia ya kujenga amani na mustakabali jumuishi.”
Amesema kwa IOM ambayo ilifurushwa Syria na utawala ulioondolewa madarakani, iliendelea kusaidia wasyria kupitia mipakani tangu mwaka 2014 na sasa imejipanga vema na itaweza kutekeleza mipango hiyo kwa kufanya yafuatayo.
Mambo matatu ya kipaumbele cha IOM Syria
Mosi, kupata takwimu sahihi kwani kuna pengo la takwimu. IOM itawezesha Umoja wa Mataifa na serikali na wadau kufahamu mahitaji ni wapi, na wapi kuelekeza zaidi misaada “kwani bila picha sahihi hatuwezi kupeleka misaada kwa ufanisi.”
Pili, kuimarisha uwepo wetu. Tangu mwaka 2018 IOM haijaweko Damascus kutokana na sintofahamu ya serikali ya Syria iliyoondolewa. “Tunaanzisha tena uwepo wetu Damascus na maeneo mengine ya Syria ili tuweza kufanya kazi yetu kwa ufanisi na kurejesha juhudi zetu za pamoja na wadau na jamii mashinani.”
Tatu, tunawasiliana kwa karibu na nchi jirani ambazo zimehifadhi raia wa Syria hadi sasa. “Tunasihi jumuiya ya kimataifa isaidie nchi hizo zinazohifadhi idadi kubwa ya raia wa Syria.”
Na wakati huo huo tunasaidia harakati za kurejea Syria kwa hiari kufuatia makubaliano ya amani. Halikadhalika kutangamana na jamii kule waliko wasyria mathalani Sudan Kusini, Rwanda, Bosnia na Herzegovina na Liberia.