Türk kutuma Syria timu ndogo ya wataalamu wa haki za binadamu
Türk kutuma Syria timu ndogo ya wataalamu wa haki za binadamu
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu Volker Türk, amesema wiki ijayo anatuma Syria timu ndogo ya maafisa wa haki za binadamu ili kusaidia watumishi wa Umoja wa Mataifa walioko nchini humo hivi sasa kuhusu masuala ya haki za binadamu.
Msemaji wa Ofisi ya Kamishna Türk , Thameen Al-Kheetan,amewaambia waandishi wa habari hii leo mjini Geneva, Uswisi kwamba timu hiyo pia inalenga kusaidia juhudi za kuhakikisha mpito wowote Syria unakuwa jumuishi na unazingatia mifumo ya sheria ya kimataifa.
“Harakati za kusaka haki dhidi ya uhalifu uliopita pamoja na kurejesha imani ya jamii zikifanyika kwenye msingi wa haki za binadamu, itakuwa ni jambo muhimu kwa mustakabali wa Syria,” amenukuliwa Kamishna Türk .
Amesisitiza kuwa hiyo ndio njia pekee ya kutatua kiwango kisichopimika cha machungu waliyovumilia watu na familia nchini kote kwa miongo mitano, hivyo basi kujenga mustakabali ambao haki za binadamu za wasyria wote zinazingatiwa na kuheshimiwa litakuwa jambo la msingi.
Watalaamu wasisitiza kuzingatiwa kwa uhuru, ujenzi wa kidemokrasia na haki za binadamu
Wakati huo huo, kundi la wataalamu huru wa haki za binadamu wametaka usaidizi wa pamoja kwa Syria wakati huu taifa hilo liko kwenye kipindi cha mpito baada ya kuangushwa kwa utawala wa Bashar al- Assad.
Taarifa yao iliyotolewa leo Geneva, Uswisi na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, OHCHR imewanukuu wakisema kipindi hiki ni cha kihistoria kwa ukanda wa Mashariki ya Kati na kinatoa fursa ya kupata amani ya kudumu, haki na maridhiano, utawala wa kidemokrasia na kurejesha kujitawala kwa Syria.
Wametaka kuheshimiwa kikamilifu kwa mipaka na eneo la Syria, wakisisitiza kuwa ukosefu wa sheria, ghasia, na ukiukwaji uliokithiri wa sheria ya kimataifa hasa ile ya haki za binadamu na ubinadamu lazima ukome.
Dunia iungane kusaidia Syria
Kundi hilo likijumuisha zaidi ya wataalamu 40 wa haki za binadamu limesema “jumuiya ya kimataifa ishirikiane kuijenga upya Syria kwa kuzingatia kanuni za kidemokrasia ya jumuishi, kuheshimu haki za binadamu za raia wote wa Syria hasa kumulika makundi madogo na yale yanayobaguliwa, wanawake, watu walio hatarini kutokana na jinsia zao, utambulisho wa jinsia, watu wenye ulemavu, watoto, wakimbizi wa ndani na wakimbiri wanaorejea.”
Jambo lingine wametaja ni haki kwa waathirika wa vitendo vya ukatili, ikiwemo mateso, ukatili wa kijinsia, kingono, waliotoweshwa na waliosafirishwa kiharamu lazima ipatikane.
Wamesisitiza uwepo wa mfumo sahihi wa mahakama unaojikita kwenye uwajibikaji, kulipa fidia, maridhiano na sio visasi.
“Wakati usaidizi wa kimataifa na ushirikiano na Syria katika kuijenga upya ni muhimu, mchakato huo usitekwe na mataifa ya kigeni,” wamesisitiza wataalamu hao na kwamba mchakato wa kisiasa uongozwe na wasyria na umilikiwa na wasyria.
Wametaka kuanzishwa kwa serikali wakilishi kupitia mchakato wazi kwa mujibu wa azimio namba 2254 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Mambo mengine muhimu
- Wasyria au wakazi wa zamani wa Syria wakiwemo wakimbizi wa kipalestina wasirejeshwe Syria kinguvu.
- Ushiriki wa wanawake kwenye ujenzi wa amani na kipindi cha mpito Syria ni muhimu.
- Wanaunga mkono safari ya Syria ya ujenzi wa mustakabali wa kidemokrasia.
- Majeshi yote ya kigeni Syria yaondoke, na uvamizi wa eneo la Syria na mashambulizi vikome
- Vikwazo dhidi ya Syria viondolewe haraka.