Kusaka amani Syria: Fursa kubwa, hatari kubwa
Kusaka amani Syria: Fursa kubwa, hatari kubwa
Kufuatia kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad nchini Syria, Jumapili ya tarehe 8 mwezi Desemba 2024, Syria imeingia katika kipindi cha sinfofahamu, na Umoja wa Mataifa utakuwa na dhima muhimu ya kuhakikisha mpito tulivu utakaosongesha hatua za kurekebisha taasisi, kuzifanya ziwe tulivu. Halikadhalika kuendeleza juhudi za kuleta pamoja makundi na pande mbalimbali ambayo yaliibuka baada ya kuanza kwa vita mwaka 2011.
Mapigano yanavyozidi kushamiri, Umoja wa Mataifa katu haujakoma kuendelea kufanya kazi ‘nyuma ya pazia’ kusaka suluhu ya kisiasa itakayoleta utu, uhuru na haki kwa wananchi wa Syria.
Hapa tunakupatia matukio muhimu ambamo kwayo Umoja wa Mataifa umetekeleza majukumu muhimu kuelekea amani stahiki nchini Syria.
2012: Juhudi za kina za amani zimeanza
Chini ya mwaka mmoja baada ya Machi 2011 maandamano yalishamiri kwenye nchi za kiarabu kudai demokrasia, mamlaka nchini Syria zilianza msako uliosababisha vurugu. Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan (1997-2006) alipatiwa jukumu la kusongesha juhudi za kutatua mzozo huo, akipatiwa nafasi ya Mjumbe Maalum wa Pamoja wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa nchi za Kiarabu, kwa ajili ya Syria.
Bwana Annan aliandaa mpango wa vipengele sita, ukitaka kumalizika kwa ghasia, mashirika ya kibinadamu kupatiwa fursa ya kufikisha misaada, kuachiliwa kwa wale waliokuwa wameswekwa korokoroni, kuanza kwa mazungumzo jumuishi ya kisiasa, na vyombo vya habari vya kimataifa vipatiwe fursa ya kufanya kazi nchini Syria.
Mpango huo uliidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi Aprili mwaka 2012, kupitia maazimio namba 2042 na 2043, na kisha kuwezesha kuanzishwa kwa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Usimamizi Syria, (UNSMIS), ambao ulidumu kwa muda mfupi tu kwani ulikoma mwezi Agosti mwka huo huo wa 2012 baada ya mapigano kushika kasi.
Mwaka 2012 pia kulichapishwa Taarifa ya pamoja ya Geneva , ikiwa ni matokeo ya mkutano wa Kundi la Hatua kwa ajili ya Syria, ambalo lilijumuisha nchi kadhaa za Mashariki ya Kati na wajumbe 5 wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Nyaraka hiyo, ilipitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Nyaraka hii ilisongesha mpango wa amani wa Bwana Annan, na tangu wakati huo imekuwa ikiongoza juhudi za usuluhishi zinazoongozwa na Umoja wa Mataifa.
2014: Mkwamo Geneva
Bwana Annan aliachia jukumu la MWakilishi Maalum mwezi Agosti mwaka 2021, na jukumu hilo likachukuliwa na mwanadiplomasia raia wa Algeria, Lakhdar Brahimi, ambaye kipindi chake kilikumbana na kuongezeka kwa mzozo na kuwa vita kamili.
Mwezi Januari mwaka 2014, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo Ban Ki-Moon aliitisha mkutano wa kimataifa ukipatiwa jina Geneva II, uliofuatiwa na mazungumzo kati ya wawakilishi wa serikali ya Syria na majeshi ya upinzani, mazungumzo haya yaliongozwa na Bwana Brahimi.
Hatimaye, pande mbili hizo haziweza kuafikiana: Brahimi alisitisha mazungumzo hayo na hakuongeza muda wa jukumu lake baada ya Mei 2014.
2015: Kupitishwa kwa azimio muhimu
Mweleko ulipatikana kiasi mwaka uliofuatia, wakati wa kipindi cha aliyepokea ‘mikoba’ ya Brahimi, Staffan de Mistura.
Mazungumzo ya kina ya kidiplomasia mwaka 2015 kati ya Urusi na Marekani pamoja na wadau wengine muhimu wa kimataifa, yaliwezesha kuanzishwa kwa Kundi la Kimataifa la Usaidizi kwa Syria (ISSG), kujadili jinsi ya kusongesha harakati za kumaliza mzozo wa Syria.
Mazungumzo hayo yaliwezesha kupitishwa kwa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 2254 la mwaka (2015), azimio hili liliweka muda wa mpito wa kisiasa, ikiwemo nashauriano ya kuanzisha serikali halali, jumuishi, isiyo ya kidini, na mchakato na muda wa kuandika katiba mpya. Halikadhalika ilitaka kuweko kwa uchaguzi huru na haki, utakaosimamiwa na Umoja wa Mataifa.
2016: Kukabliana na ukwepaji sheria kwa uhalifu wa kivita na ukatili
Ukwepaji sheria umekuwa ndio alama ya mzozo wa Syria. Umekwamisha utatuzi wa mzozo na umekuwa changamoto kubwa kwa maadili ya msingi ya Umoja wa Mataifa ambayo ni uwajibikaji.
Wakati wote wa mzozo, Umoja wa Mataifa umefanya kazi kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu na kufuatilia vikundi vya kigaidi: Azimio namba 2254 linasisitiza wito wa awali wan chi wanachama kukabiliana na vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na kikundi cha Islamic State nchini Iraq na kile cha Levant (ISIL) kikijulikana pia kama Dae’sh. Vikundi vingine ni Al-Nusra Front, Al Qaeda na mengineyo, na kutoa wito kwa pande kwenye mzozo huo kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingizwa, kuachiliwa huru kwa waliokamatwa kiholela, hasa wanawake na watoto.
Hatua muhimu katika kutatua suala la ukwepaji sheria ilichukuliwa tarehe 21 Desemba 2016, wakati Kamisheni ya Kimataifa Isiyoegemea upande wowote na iliyo huru, (IIIM) ilianzishwa kupitia azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
IIIM ilianzishwa kusaidia uchunguzi na kushtaki uhalifu mbaya zaidi, hasa uhalifu unaohusiana na mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita.
Tarehe 8 Desemba, 2024, taarifa kuhusu kuanguka kwa utawala wa Assan zilizotawala vichwa vya habari, IIIM ilitoa taarifa ikielezea matumaini kwamba hatimaye wasyria watapata fursa ya kuishi kwenye nchi yao kwa misingi ya haki na utawala wa kisheria.
“Uwajibikaji kwa machungu yasiyohesabika kwa zaidi ya miaka 13 unapaswa kuwa kitovu cha majadiliano ya mustakabali wa Syria, na juhudi za wasyria na jumuiya ya kimataifa vivyo hivyo… kuanza kutatua suala la ukwepaji sheria kwa ukatili wowote ule usiofikirika: kuanzia kushambulia hospitali, kutumia silaha za kemikali, utesaji uliopangwa na serikali kwenye magereza yaya serikali, kusambaa kwa ukatili wa kingono na kijinsia na hata mauaji ya kimbari.”
2024: Zama mpya za matumaini na ukosefu wa uhakika
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alitangaza Jumapili Desemba 8, kwamba “kuanguka kwa utawala wa kidikteta ni fursa ya kihistoria kwa wasyria kujenga mustakabali tulivu na wa amani,” ingawa alisisitiza kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha mpito wa kisiasa wenye utaratibu ili kurejesha upya taasisi.
Mjumbe wake Maalum kwa Syria, mwanadiplomasia Geir Pedersen kutoka Norway– aliteuliwa kushika wadhifa huo Oktoba 2018. Yeye ametoa wito kwa “mazungumzo ya dharura ya kisiasa” mjini Geneva, Uswisi, “kujadili mustakabali wa Syria,huku akisema kwamba nchi muhimu kwenye suala hilo ambazo ni Iran, Russia, Uturuki na Marekani, zimeunga mkono ombi hilo.
“Zama hizo za giza zimeacha makovu makubwa,” amesema Bwana Pedersen akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumapili. “Lakini leo tuna matumaini yenye tahadhari, tukifungua ukurasa mpya – ukarasa wa amani, maridhiano, utu na ujumuishi kwa wasyria wote.”
Bwana Pedersen pia amesema hakuna kinachopaswa kuzuia mpito wenye amani. Kukiweko mamlaka zilizojitwalia uongozi kikiwemo kikundi cha HTS ambacho kiliongoza kuanguka kwa serikali ya Syria katika baadhi ya maeneo ya nchi, kuna makundi mengine yanayoendesha shughuli zao ndani ya Syria.
Hali bado ni tete, na Mjumbe Maalum amesisitiza wakati akihutubia Baraza la Usalama lililokutana kwa faragha tarehe 9 Desemba 2024, kwamba: “Kuna fursa halisi ya mabadiliko, lakini fursa hii inahitaji kutumiwa na wasyria wenyewe na kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa na jumuiya ya kimataifa.”
Syria na UN |
|